Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amewasihi wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu, ili kuwachagua viongozi watakaosimamia na kutetea maslahi yao.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo, Alhamisi, Nyamhokya amesema ni muhimu wafanyakazi kutimiza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura kwa kuwa ndiyo msingi wa kupata viongozi wanaosikiliza sauti zao na kuwajali.
“Nitumie fursa hii kuwasisitiza kuendelea kuwashawishi wafanyakazi wa Arusha na Tanzania nzima tujitokeze kwa wingi Oktoba 29, kwenda kupiga kura ili tuwachague viongozi wanaojali maslahi yetu,” asema.
Amesema nchi ipo salama, hivyo hakuna sababu kwa wafanyakazi kutojitokeza, akisisitiza kuwa siku ya kupiga kura itakuwa ya mapumziko, hivyo kila mmoja ahakikishe anashiriki kabla ya kuendelea na shughuli zake nyingine.
“Kapigeni kura Oktoba 29, tuwachague viongozi ambao tunapozungumza nao mambo yetu yanatekelezwa. Tunahitaji viongozi wanaosikiliza sauti za wafanyakazi,” amesisitiza Nyamhokya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED