UDP ikishika dola itatetea haki za wanawake, kujaza watanzania fedha

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 12:11 PM Aug 15 2025
Saum, akiwa na mgombea mwenza wake, Juma Khamis Faki, alisema kuwa watawajaza fedha Watanzania kwa kufungua fursa mbalimbali katika sekta za kilimo, kuboresha miundombinu, pamoja na kuongeza idadi ya wataalamu katika sekta ya elimu.

Chama cha United Democratic Party (UDP) kimesema endapo kitapewa ridhaa ya kushika dola, kitawajaza Watanzania fedha ili waweze kujikomboa kiuchumi, huku kikisisitiza pia suala la haki za wanawake katika uongozi pamoja na jitihada za kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Kauli hiyo imetolewa leo, Agosti 15, 2025, na mgombea wa urais kwa tiketi ya chama hicho, Saum Hussein Rashid, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais katika ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) zilizopo Njedengwa.

im

"Tunaposema kuwajaza fedha Watanzania, tuna maana ya kuweka miundombinu mizuri kwa wananchi ili waweze kupata fedha zitakazowaainua kiuchumi. Kwa mfano, zao la pamba litafanyiwa maboresho kwa kutumia mbinu za kisasa, pamoja na mazao mengine," amesema Saum.

Ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuboresha miundombinu ya wananchi na kuwezesha kilimo chenye tija, jambo litakalofungua fursa za biashara na kuongeza mapato kwa wananchi.

Kuhusu haki za wanawake katika uongozi, Saum Hussein Rashid amebainisha kuwa UDP itahakikisha wanawake wanapewa nafasi sawia za kushiriki uongozi na pia itachukua hatua za kudhibiti na kutokomeza ukatili wa kijinsia nchini.