MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imesema imejikita katika kuwainua wajasirimali ikiwamo mafundi, wafugaji na wavuvi, ili waajiri na waajiriwe kwenye sekta mbalimbali.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Anthony Kasore, alisema hayo akizungumza na waandishi wa habari jana, kwenye Banda la VETA katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) maarufu Sabasaba.
Amesema kwa mwaka huu, VETA imekuja na dhana za kilimo zinazorahisisha kazi kwa wakulima na wafugaji, ikiwamo ya kutengeneza chakula cha mifugo na inayopukuchua mahindi.
“Tumekuna na mashine za ‘incubators’ inayoweza kutotoresha vifaranga ikitumia nishati ya jua, pamoja na bidhaa ambazo zinafukuza mbu. Lengo kusaidia jamii wapate ujuzi na kwenda kuuza bidhaa wakizalisha,” amesema.
Amesema hivi sasa VETA imefungua kampuni rasmi ambayo inauza bidhaa zinazotengenezwa na mamlaka hiyo, pia waliopata ujuzi huweza kuzipata bidhaa hizo, ili wakazalishe vitu tofauti kama vile sabuni.
“Lakini mwaka huu pia tumetenga eneo maalum kwa ajili ya watoto,ili wajue umuhimu wa ujuzi na ubunifu. Sera ya Elimu Tanzania, imefanyiwa maboresho na mwaka 2025 Februari, Rais aliizindua,” amesema Kasore.
Amesema wakati sera hiyo ikija na mafunzo ya amali, upo umuhimu wa jamii kujua kwamba watoto wanapaswa kufahamu ufundi mdogo tangu wadogo.
Kadhalika, amesema wapo waliohitimu elimu ya juu, wamerudi VETA kupata mafunzo ya amali ambayo yamewafanya wakajiajiri.
“Tunatengeneza majiko kutumia nishati safi, ili kuungana na jitihada ya Rais Samia kupunguza athari za matumizi nishati isiyotinza mazingira,” ameongeza Kasore.
Amesema nchini tayari kuna 80 vimejemgwa, huku 65 vikitarajiwa kujengwa kwa fedha ya Sh. bil 100 zikitumika na kisha kufanikisha kila wilaya kuwa na chuo cha VETA.
“Kila wilaya kulingana na aina ya shughuli inayofanyika hapo, tutatoa mafunzo ya uvuvi kwenye uvuvi na madini kama kuna uchimbaji madini,” amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED