Vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini wamekutana jijini Mwanza kwa lengo la kuwahamasisha wenzao kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu ujao, ili kuonyesha ujasiri na kutumia sauti yao kumchagua kiongozi sahihi.
Kongamano hilo la vijana lililofanyika jijini humo limeangazia umuhimu wa ushiriki wa vijana katika mchakato wa uchaguzi, sambamba na kudumisha amani ambayo imetajwa kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.
Wakizungumza katika kongamano hilo, washiriki walisisitiza kuwa vijana wana nafasi ya kipekee katika kuamua hatima ya taifa kupitia kura zao.
Pendo Msote, mmoja wa vijana waliohudhuria, alisema kuwa vijana ni nguzo kuu ya taifa, hivyo ni wajibu wao kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu.
“Sisi vijana tunayo nafasi kubwa ya kubadili hatima ya nchi yetu kwa kuchagua viongozi bora,” alisema Msote. “Hatutaki kuona amani yetu inavunjwa, hivyo ni muhimu tushiriki kwa wingi katika uchaguzi.”
Kwa upande wake, Kashinje John alifafanua kuwa kura ni sauti ya kila kijana na ni chombo muhimu cha kuleta mabadiliko chanya katika taifa.
“Kura yako ni sauti yako, na ni njia ya kuwakilisha wale ambao hawana fursa ya kupiga kura. Kura moja inaweza kuamua mustakabali wa taifa letu,” alisema Kashinje.
Aidha, vijana walihimizwa kulinda amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
“Amani ni urithi wetu. Tunaweza kuichukulia kama kitu cha kawaida, lakini ni hazina kubwa isiyopaswa kuchezewa,” aliongeza Kashinje.
Kwa mujibu wa Ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume Huru ya Uchaguzi imepewa jukumu la kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki, uhuru na amani. Kura imeelezwa kuwa si tu haki bali pia ni wajibu wa kila Mtanzania, hasa vijana, kuchangia katika kuunda taifa bora.
Naye aliyewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisisitiza kuwa uchaguzi ni tukio la kihistoria linaloonyesha dhamira ya Watanzania katika kudumisha demokrasia, utulivu na amani.
“Siku ya kupiga kura ni siku takatifu ni siku ambayo Tanzania hujionyesha kwa mataifa mengine kama taifa lenye demokrasia, utulivu na amani,” alisema Nyalandu.
Ameongeza kuwa Tanzania ni mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika kutokana na amani na utulivu wake wa kipekee.
“Hii ni amani ya thamani kubwa ambayo tunapaswa kuilinda kwa gharama yoyote,” alihitimisha Nyalandu.
Katika hitimisho la kongamano hilo, vijana walijipanga kuendelea kuhamasishana kuhusu umuhimu wa kushiriki kwenye uchaguzi, wakisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kutekeleza wajibu wao wa kiraia na kuchangia katika ujenzi wa taifa lenye misingi imara ya kidemokrasia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED