Msukumo wa Tanzania kuelekea kilimo cha kisasa unazidi kuimarika, baada ya wadau muhimu wa kitaifa kukutana jijini Dodoma, kwa ajili ya Mkutano wa Wadau wa Umekanishaji.
Mkutano huo wa ngazi ya juu ulilenga kuweka mpango wa pamoja kupanua matumizi ya mashine za kisasa, kuongeza ushiriki wa vijana na wanawake na kuelekeza maeneo ya uwekezaji wa baadaye katika sekta ya kilimo.
Utafiti wa Soko uliofanywa na AgriFrontier East Africa na kuwasilishwa na AGRA kupitia TAPBDS, mshirika mkuu wa umechanishaji nchini Tanzania, umeonesha ongezeko kubwa la matumizi na mahitaji ya mashine za kisasa na fursa pana kwa vijana na wanawake.
Utafiti huo umeutaja mkoa wa Manyara kama mkoa wenye matumizi makubwa yam ashine za kilimo na watumiaji wakubwa ni wanawake.
Katika mjadala wa wazi, vijana washiriki walieleza changamoto zinazowakabili, ikiwemo ukosefu wa mtaji, gharama kubwa za mashine na pengo la ujuzi wa hali ya juu unaowazuia kushindana kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa umechanishaji.
Wengi wao walisisitiza kuwa mfumo wa Lease-to-Own (ukodishwaji) ndio njia rafiki zaidi kwao kuingia kwenye biashara ya mechanization, huku wakitaka taasisi za fedha kupunguza kiwango cha malipo ya awali ili kuufanya kuwa rafiki kwa vijana.
Taasisi kama SIDO na VETA zilieleza kuwa, licha ya mafunzo wanayotoa kwa vijana katika uendeshaji na utengenezaji wa mashine, bado idadi kubwa ya vijana wanao hitimu huishia kutafuta ajira badala ya kuanzisha biashara, hasa kutokana na uhaba wa mtaji wa kuanzia na ukosefu wa usaidizi wa kibiashara.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti, Mkurugenzi Mtendaji wa TAPBDS, Joseph Migunda, amesema matokeo hayo yanaashiria hatua muhimu ya mabadiliko katika sekta ya kilimo nchini.
“Ushahidi unaonesha wazi kwamba mechanization inaweza kufungua maelfu ya fursa kwa vijana na wanawake,” amesema.
“Kuna mahitaji makubwa ya mashine, hamasa inayoongezeka ya huduma zinazoongozwa na vijana na ubunifu.
Tukipata sera sahihi na uwekezaji unaolenga matokeo, vijana na wanawake wanaweza kuwa uti wa mgongo wa kilimo cha kisasa chenye tija kubwa.”
Ameongeza kuwa mifano ya biashara iliyojaribiwa hapa nchini tayari imeonyesha mafanikio katika kupunguza kazi ya mikono, kuongeza ufanisi na kuboresha kipato cha kaya za vijijini.
Mgeni rasmi Mhandisi Anna Mwangamilo, Mkurugenzi wa Zana za Kilimo na Uongezaji Thamani katika Wizara ya Kilimo, amesisitiza dhamira ya serikali ya kuendeleza kilimo chenye tija na ushirikishwaji.
Amesema Tanzania inalenga zaidi ya asilimia 10 ya ukuaji wa kilimo kwa mwaka kufikia 2030 na kwamba mechanization ndio chombo muhimu cha kuongeza uzalishaji, kupunguza upotevu wa mazao na kufikia lengo la mauzo ya nje ya dola bilioni tano za Marekani.
Katika tangazo muhimu, Anna amesema serikali itagawa matrekta 500 na mashine 800 za kukoboa mazao mahsusi kwa vijana na wanawake wanaojishughulisha na kilimo.
“Mechanization si kifaa tu ni injini ya mabadiliko,” amesema.
“Tunaweka msingi wa mageuzi kupitia tafiti za uhakika, na tunataka vijana na wanawake wawe kitovu cha safari hii ya kisasa.”
Ameongeza kuwa serikali imefurahishwa na mifumo ya biashara iliyopendekezwa, vikundi vya vijana vinamiliki mashine ndogo na kutoa huduma kwa wakulima wengine.
Amethibitisha kuwa wizara imewaalika AGRA na TAPBDS kujadiliana zaidi kuhusu namna ya kuingiza mifumo hiyo katika mpango wa kitaifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED