Waandishi wa IPP Media wang’ara Tuzo za Mawasiliano 2025

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 03:58 PM Aug 08 2025
Waandishi wa IPP Media wang’ara Tuzo za Mawasiliano 2025
Picha: Mpigapicha Wetu
Waandishi wa IPP Media wang’ara Tuzo za Mawasiliano 2025

Waandishi wa Habari kutoka Kampuni ya IPP Media wameibuka washindi katika Tuzo za Mawasiliano zilizofanyika Agosti 7, 2025 katika Ukumbi wa Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Zanzibar.

Tuzo hizo zilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa SMZ, Sharif Ali Sharif, ambapo waandishi wa IPP Media walitamba kwa kuchukua tuzo mbalimbali katika vipengele tofauti vya uandishi wa habari.

Farouk Karim wa ITV aliongoza kwa kutwaa tuzo tatu — mshindi wa kwanza kwenye kipengele cha Televisheni, mshindi wa pili kwenye Televisheni (kwa kazi tofauti), na mshindi wa pili katika Mitandao ya Kijamii.

Kwa upande wa magazeti, Rahma Suleiman wa Gazeti la Nipashe alishika nafasi ya tatu, huku Halfan Chusi, anayehusika na habari za mtandaoni, akiibuka mshindi wa nne katika kipengele cha habari za mtandaoni kupitia Nipashe Digital.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Waziri Sharif alisisitiza mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi, hasa kuhusu shughuli na mafanikio ya serikali.

"Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua na kuthamini nafasi muhimu ya vyombo vya habari katika kusukuma mbele maendeleo ya nchi. Ushirikiano na wanahabari utazidi kujenga jamii yenye uelewa mpana, uwazi na mshikamano," alisema Waziri Sharif.

Aidha, aliwapongeza washindi wote kwa kazi zao bora zinazochangia kudumisha amani, utulivu na maendeleo, akibainisha kuwa tuzo hizo ni sehemu ya kutambua kazi nzuri ya wanahabari katika kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nane (Zanzibar) na Awamu ya Sita (Tanzania Bara).