Wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani wameeleza kuridhishwa kwao na hali ya huduma ya maji inayotolewa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), wakisema imeendelea kuimarika na kuwahakikishia usalama wa matumizi ya maji hayo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema juhudi zinazofanywa na DAWASA kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali zimeleta faraja kubwa, kwani changamoto za awali zimepungua kwa kiasi kikubwa.
Ibrahim Isanja, mkazi wa mtaa wa Kilungule, kata ya Kimara, amesema huduma ya maji kutoka DAWASA imekuwa mkombozi mkubwa kwao, kwani kwa sasa hawana mbadala mwingine wa huduma hiyo.
“Siku chache zilizopita kulizuka taharuki kuhusu usalama wa maji tunayoyatumia, lakini tumeendelea kuyatumia bila kupata madhara yoyote. Naipongeza DAWASA kwa kuwa wa kwanza kuwahakikishia wananchi kwamba maji haya ni salama kwa matumizi,” amesema Isanja.
Naye Zainabu Issa, mkazi wa Mbezi, amewatoa hofu wananchi akisisitiza kuwa maji yanayotolewa na DAWASA ni safi na salama kwa matumizi ya kila siku.
“Napenda kuwashauri wananchi wenzangu kwamba pindi taharuki ikitokea, tuwe na subira na tusubiri taarifa sahihi kutoka kwa mamlaka husika. Mimi na familia yangu tunatumia maji haya kila siku bila matatizo yoyote,” amesema Zainabu.
Kwa upande wake, Andrew Frank, mkazi wa Zinga, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani, amesema huduma ya maji katika eneo lao imekuwa ya uhakika na haina changamoto yoyote.
“Kwa sasa maji yanapatikana wakati wote, na hakuna mtu yeyote ninayemfahamu aliyepata madhara kutokana na matumizi ya maji haya. Tunamshukuru DAWASA kwa huduma bora,” amesema Frank.
Huduma bora ya maji katika maeneo ya Dar es Salaam na Pwani ni sehemu ya mpango endelevu wa DAWASA wa kuhakikisha kila kaya inapata maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na shughuli za kiuchumi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED