Mgombea ubunge wa Jimbo la Kivule kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Wakili Peter Madeleka, amesema iwapo atashinda katika uchaguzi mkuu ujao ataweka nguvu kubwa kusaidia wananchi kutatua kero mbalimbali zilizoshindikana kwa muda mrefu, akisisitiza kwamba uzoefu wake wa kisheria utakuwa nyenzo muhimu ya kuishinikiza serikali kutekeleza majukumu yake.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Madeleka alisema anatambua changamoto zinazowakabili wananchi wa Kivule, ikiwamo ubovu wa miundombinu, ukosefu wa ajira, matatizo ya elimu na huduma za afya duni, na ameahidi kuzifanyia kazi kwa kipindi cha miaka mitano.
Vipaumbele vyake
Madeleka alisema vipaumbele vyake vitajikita katika maeneo ya elimu, afya, ajira, miundombinu, uwajibikaji na mazingira.
📌Kauli mbiu ya kampeni
Madeleka amesema kampeni yake inabebwa na kauli mbiu ya “Maendeleo kwa Wote, Uwajibikaji Kwanza”, akisisitiza kwamba hata kabla ya kuchaguliwa tayari amekuwa akitatua changamoto za wananchi wa Kivule.
Ametaja kuwa kwa sasa anashughulikia zaidi ya kesi 17 za migogoro ya ardhi na kesi 32 za mirathi kwa wananchi wa jimbo hilo, huku pia akisaidia familia ambazo ndugu zao wamekwama hospitalini kwa kushindwa kulipa gharama za mazishi.
“Kwa sababu mimi ni wakili, sihitaji kusubiri mpaka nishinde ndiyo nianze kutatua matatizo ya wananchi wangu. Tayari nipo nao kwenye kesi za ardhi na mirathi, na hata kuhakikisha maiti zilizokwama hospitalini zinapata heshima ya kuzikwa,” amesema.
📍Michezo na Vijana
Madeleka pia ameahidi kuendeleza michezo kwa kushirikiana na serikali kutenga maeneo ya vijana kufanyia michezo, akibainisha kuwa michezo ni ajira na chanzo cha kipato.
📍Anataka kuacha alama
“Nataka kuacha alama ya haki na maendeleo. Wananchi wa Kivule wakienda hospitali wapate huduma bora, akina mama wajifungue salama, migogoro ya ardhi ikome na vijana wapate ajira. Naomba wananchi wanipatie ridhaa, nitasimama kwa niaba yao bungeni,” amesema Madeleka.
Amehitimisha kwa kuwataka wananchi wa Kivule kuhudhuria kwa wingi mkutano wa uzinduzi wa kampeni zake Kata ya Majohe – Ngonzoma, ambapo kutakuwa na burudani za wasanii, chakula na vinywaji, sambamba na kusikiliza sera na vipaumbele vyake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED