Chama cha Hisabati Tanzania (MAT/CHAHITA) kimetangaza matokeo ya Mtihani wa Mashindano ya Kitaifa ya Hisabati (TAMO) mwaka huu, yakionesha wavulana kuongoza kwa kupata alama za juu ukilinganisha na wasichana.
Akizungumza mjini Dodoma, Mwenyekiti wa chama hicho, Dk. Said Sima, alisema mtihani huo ulifanyika Agosti 8, 2025, na kushirikisha wanafunzi 1,736 wa kidato cha tatu, nne, tano na sita kutoka mikoa 18 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Kati ya washiriki hao, wanafunzi wa kidato cha tatu na nne walikuwa 1,117. Wanafunzi waliopata alama zaidi ya asilimia 40 walikuwa 172, ambapo wavulana walikuwa 112 (asilimia 65) na wasichana 60 (asilimia 35). Aidha, wanafunzi 448 (asilimia 40.1) walipata alama kati ya asilimia 20–39, huku wavulana wakiwa 212 (asilimia 47) na wasichana 236 (asilimia 53). Waliopata chini ya asilimia 20 walikuwa 497, akiwemo wavulana 233 na wasichana 264.
Kwa upande wa wavulana waliotajwa kuongoza katika kidato cha tatu na nne ni Goodluck Lyali (Ilboru-Arusha) aliyeibuka mshindi wa kwanza kitaifa, akifuatiwa na Yohana Nsila (Mzumbe-Morogoro), Silvanus Alfred, Mikidadi Misai (Marian Boys-Pwani) na Vicent Vicent (Mahina-Mwanza).
Kwa upande wa wasichana, waliobainika kufanya vizuri ni pamoja na Nasra Shabani (St. Monica Girls–Arusha), Zalwango Ange (White Lake-Dar es Salaam), Amaro Hiza, Elina Mhagama, Gladness Mbena (St. Francis-Mbeya), Sharon Anania (Feza Girls-Dar es Salaam) na Josephine Shayo (St. Francis-Mbeya).
Kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita, jumla ya 619 walipata alama zaidi ya asilimia 40. Wanafunzi 109 (asilimia 17.6) walipata alama kati ya asilimia 20–39, ambapo wavulana walikuwa 82 (asilimia 75) na wasichana 27 (asilimia 25). Aidha, waliopata alama chini ya asilimia 20 walikuwa 240, wakiwemo wavulana 143 (asilimia 59.6) na wasichana 97 (asilimia 40.4).
Wavulana waliotajwa kuongoza katika kundi hili ni Zacharia Mwita (Ilboru-Arusha), Henry Rulagirwa (Tabora Boys), Reward Mbutta (St. Peter Claver-Dodoma) na Japhet Kagosha (Karatu-Arusha). Kwa upande wa wasichana waliofanya vizuri ni Irene Kissima, Zalha Hamza (Msalato-Dodoma), Anisa Issa, Ummul Mohamed (Lumumba-Zanzibar), Joyce Wambura (Kilakala-Morogoro) na Mary Mawalla (Loleza-Mbeya).
Dk. Sima alisema mashindano haya hufanyika kila mwaka kwa ushirikiano na Idara ya Hisabati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), yakiwa na lengo la kuibua na kutambua vipaji vya wanafunzi, kuongeza hamasa na ufaulu wa hisabati, pamoja na kuandaa vijana kushiriki mashindano ya kimataifa.
Aliongeza kuwa mashindano hayo pia yanasaidia kuleta ushindani wa mbinu za kujifunza somo hilo, kutambua vipaji na kuviendeleza. Aidha, alimshukuru Mfadhili Mkuu wa mashindano hayo, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa mchango wake katika kukuza elimu ya hisabati nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED