RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, leo amewaapisha mawaziri na manaibu mawaziri aliowateua, huku akisisitiza kwa mara nyingine umuhimu wa kuimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa maslahi ya nchi.
Hafla ya uapisho huo ilifanyika katika Viwanja vya Ikulu Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, dini, vyama vya siasa pamoja na familia za mawaziri na manaibu waziri hao.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Mwinyi alisema bado anaamini kuwa matakwa ya kikatiba yanaruhusu na kutaka uwepo wa SUK, hivyo akakitaka chama kilichoshika nafasi ya pili katika uchaguzi mkuu kwa kupata zaidi ya asilimia 10, ACT Wazalendo kutathmini umuhimu wa kushiriki katika serikali hiyo kwa ajili ya umoja wa nchi na wananchi.
Alisema kuwa SUK ni kwa maslahi mapana ya Zanzibar, hivyo ni vyema kufikiwa muafaka ili kuunda serikali madhubuti yenye umoja na uwiano wa kitaifa.
Akitoa msisitizo kwa Mawaziri Dk. Mwinyi aliwataka viongozi hao wapya kutambua kuwa huo si wakati wa kusherehekea, bali ni muda wa kujipanga kutekeleza majukumu ya wananchi.
“Ni wajibu wetu kuhakikisha tunatimiza malengo ya maendeleo ya Zanzibar pamoja na Dira ya Maendeleo ya 2050,” alisema. Alieleza kuwa katika awamu yake ataendesha tathmini za mara kwa mara kwa kila wizara ili kuhakikisha malengo ya serikali yanatekelezwa ipasavyo.
Aidha, aliwataka mawaziri kujua muundo wa wizara zao na kuandaa mpango kazi mahsusi utakaotekeleza Dira ya 2050, mpango wa maendeleo na Ilani ya CCM.
Azungumzia matumizi ya fedha na safari
Dk. Mwinyi alisema maeneo ya fedha na makusanyo hayakufanya vizuri katika awamu iliyopita, hivyo akazitaka wizara kuboresha mifumo ya ukusanyaji na kuhakikisha makusanyo yanaendana na matumizi yenye tija.
Aliongeza kuwa safari na mafuta ni maeneo yanayotumia fedha nyingi za serikali, hivyo safari zisizo na tija hazitaruhusiwa.
“Kama huwezi kuamua safari zenye tija, na zisizo na tija, nitakuamulia mimi,” alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED