BURIANI MUHAMMADU BUHARI; Kiongozi mjeshi kwa kupindua

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:56 PM Jul 16 2025
Muhammadu Buhari enzi za uhai wake
Picha: Mtandao
Muhammadu Buhari enzi za uhai wake

NIGERIA ni taifa lililoandika historia ya kuongozwa na wanajeshi kwa miaka 33 mfululizo tangu mwaka 1966 hadi 1999. Ni wakati ambao jeshi lilikuwa likipindua, kuua, kuchukua madaraka na kudhibiti serikali.

Ni enzi  iliyotawaliwa na mfululizo wa mapinduzi lakini wale waliopindua wakigeuziana kibao na kupindua wenzao, ikiwa ni kama kila wiki kuna mapinduzi na mfululizo wa viongozi wa kijeshi majenerali kila mwaka kuuawa, kuua, au kukimbia nchi.

Uongozi wa kwanza wa kijeshi ulianza na mapinduzi yaliyofanywa na Johnson Aguiyi-Ironsi. Huyu alipinduliwa na kuuawa na Jenerali Yakubu Gowon, ambaye pia hakudumu akaangushwa na  Murtala Muhammed.

Mapinduzi yaliendelea baada ya Murtala Muhammed kuawa,  Olusegun Obasanjo,akachukua nchi, naye akaangushwa na  Muhammadu Buhari, ambaye alipinduliwa na Ibrahim Babangida ambaye aling’olewa na Sani Abacha aliyefariki dunia na  uongozi wa kijeshi ukawa chini ya Abdulsalami Abubakar, aliyemalizia zama hizo.

Jenerali obasanjo ni kiongozi wa kwanza mjeshi aliyeongoza serikali ya kiraia, akigombea na kupigiwa kura akawa Rais wa Nigeria wa kuchaguliwa mwaka 1999.

Kiongozi mwingine ni Meja  Jenerali Muhammadu  Buhari(82), ambaye alifariki juzi jijini London, Uingereza . Aliingia madarakani Mei  2015 hadi  2023.

Itakumbukwa kuwa alikuwa kiongozi wa kijeshi wa Nigeria kuanzia  Desemba 1983 hadi Agosti 1985  kwa kipindi cha miezi 20 pekee kisha kupinduliwa.

HISTORIA

Muhammadu Buhari (82) aliyefariki Jumapili, alizaliwa Desemba 1942 huko Daura, Katsina kaskazini mwa Nigeria, karibu na mpaka wa Niger. Wakati huo, Nigeria ikiwa chini ya ukoloni wa  Waingereza na ilikuwa miaka 18 zaidi kabla ya kupata uhuru.

Buhari baada ya kumaliza shule ya msingi na sekondari, alisoma katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Nigeria, akijiunga na jeshi muda mfupi baada ya uhuru, akisoma zaidi Uingereza kuanzia 1962-1963 na kisha akaanza kupanda vyeo.

Katika miaka ya baadaye, Buhari alihusisha mwelekeo wake wa nidhamu na kutumia miaka yake ya kielimu katika shule ya bweni, ambapo adhabu ya viboko ilikuwa ya kawaida, na katika jeshi. Alikuwa na "bahati" kupata uzoefu wa mazingira magumu kama haya, ambayo yalimfundisha kufanya kazi kwa bidii.

Mnamo 1966, kulikuwa na mapinduzi ya kijeshi, lakini  daima alishikilia kuwa alikuwa mdogo sana kuwa na jukumu lolote muhimu, baada ya miaka 10 chini ya serikali ya kijeshi, Buhari aliinuka na kuwa gavana wa kijeshi wa kaskazini-mashariki, akiongoza majimbo sita.

Baada ya chini ya mwaka mmoja, Buhari, ambaye wakati huo akiwa na umri wa kati ya miaka 30, alipandishwa cheo tena, na kuwa kamishna wa shirikisho wa petroli na maliasili (kama waziri wa mafuta) mwaka 1976 chini ya Olusegun Obasanjo katika kipindi chake cha kwanza kama mkuu wa nchi wa Nigeria.

UONGOZI KIJESHI 

Mwishoni mwa 1983 kulitokea mapinduzi dhidi ya rais mteule Shehu Shagari, na Buhari, ambaye wakati huo alikuwa meja jenerali, akawa mtawala wa kijeshi wa Nigeria. Kwa maelezo yake  hakuwa mmoja wa wapanga njama lakini aliwekwa na hatimaye kutupwa na wale waliokuwa na mamlaka halisi.

Ripoti nyingine zinaonesha alikuwa na jukumu kubwa katika kumwondoa Shagari kuliko alivyokuwa tayari kukiri.Alitawala kwa muda wa miezi 20, kipindi ambacho kinakumbukwa kwa kampeni dhidi ya utovu wa nidhamu na ufisadi, pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Takribani wanasiasa 500, maofisa na wafanyabiashara walifungwa jela kama sehemu ya kampeni dhidi ya ubadhirifu na ufisadi. Wengine waliona kuwa ni ukandamizaji wa utawala wa kijeshi. Wengine wanakumbuka kama jaribio la kusifiwa la kupambana na ufisadi ulioenea ambao ulikuwa unarudisha nyuma maendeleo ya Nigeria.

Buhari alidumisha sifa adimu ya uaminifu miongoni mwa wanasiasa wa Nigeria, wanajeshi na raia, hasa kwa sababu ya kampeni hii. Kama sehemu ya vita dhidi ya utovu wa nidhamu, aliamuru Wanigeria kupanga foleni kwenye vituo vya mabasi, chini ya macho makali ya askari wanaotumia mijeledi. 

Watumishi wa umma waliochelewa kazini walidhalilishwa hadharani kwa kulazimishwa kurukaruka kichura. Baadhi ya hatua zake zinaweza kuonekana kuwa za kificho tu. Lakini nyingine zilikuwa za ukandamizaji wa kweli, kama vile amri ya kuzuia uhuru wa vyombo vya habari, ambapo waandishi wa habari walifungwa.

ALIFELI WAPI

Buhari alikuwa mtawala wa kijeshi lakini aliyejinasibu kuwa mwanademokrasia alirejea madarakani kupitia uchaguzi mkuu . Licha ya kwamba alijitahidi kuwashawishi Wanigeria kwamba angeweza kuleta mabadiliko aliyoahidi mambo mepesi.

Kwa asili  hakuwa mwanasiasa, alionekana kama mtu asiye na hisia lakini mkali, alibaki na sifa ya uaminifu  jambo adimu kwa mwanasiasa nchini Nigeria.

Baada ya majaribio matatu  ya kugombea urais na kushindwa  Buhari alipata ushindi wa kihistoria mwaka 2015, na kuwa mgombea wa kwanza wa upinzani nchini humo kumshinda Rais aliyeko madarakani, akimuangusha Goodluck Jonathan.

Ilipofika  2019, alichaguliwa tena kwa muhula mwingine wa pili kwa kuongoza tena miaka mine hadi alipoondoka 2023.

IMANI ILIPOTOKEA

Wengi wa waliomuunga mkono walidhani historia yake ya kijeshi na sifa za kinidhamu ndizo ambazo nchi ilihitaji kukabiliana na uasi wa Boko Haramu kaskazini. 

Buhari pia aliahidi kukabiliana na rushwa na upendeleo serikalini na kuunda fursa za ajira kwa vijana wa Nigeria.Lakini muda wake madarakani uliambatana na kuporomoka kwa bei ya mafuta duniani na mzozo mbaya zaidi wa kiuchumi nchini humo.

Utawala wake pia ulishutumiwa kwa namna ulivyokuwa ukishughulikia ukosefu wa usalama. Wakati akifanya kampeni aliahidi kulishinda kundi la wapiganaji wa Boko Haram. Lakini kundi hilo linasalia kuwa tishio nchini humo.

Pia kulikuwa na ongezeko la mapigano makali kati ya wakulima na wafugaji wa kabila la Fulani katikati mwa Nigeria. Buhari, Mfulani, alishutumiwa kwa kutochukua hatua za kutosha kwa wafugaji au kufanya juhudi za kutosha kukomesha mzozo huo.

Shughuli za wanaojiita majambazi katika eneo la kaskazini-magharibi mwa nchi zilishuhudia kutekwa nyara kwa mamia ya wanafunzi wa shule za sekondari ya Chiboku. Lakini, vikosi vya jeshi vilishutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu kama vile kuwafyatulia risasi waandamanaji waliokuwa wakipinga ukatili wa polisi kwenye lango la tollgate  Lekki huko Lagos mnamo Oktoba 2020.

BBC SWAHILI

 

PICHA:

M. PICHA: MTANDAO