Dira ya Taifa ya 2050, sauti ya taifa kwa vizazi vyake

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:33 PM Jul 16 2025
Rais Samia Suluhu Hassan, akizindua Sera ya Mambo ya Nje hivi karibuni, kesho anatarajiwa kuzindua Dira ya Taifa ya 2050
Picha: IKULU
Rais Samia Suluhu Hassan, akizindua Sera ya Mambo ya Nje hivi karibuni, kesho anatarajiwa kuzindua Dira ya Taifa ya 2050

KESHO Julai 17, Tanzania itaandika historia. Japo ni siku ya kawaida katika kalenda ya taifa cha muhimu ni kuwa taifa litajivika tena joho la matumaini, katika njia ya pamoja kuelekea kesho iliyo bora zaidi.

Ndiyo wakati wa uzinduzi rasmi wa Dira ya Taifa ya 2050, itakayozinduliwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, mbele ya  mamilioni ya Watanzania na kuweka uelekeo mpya kihistoria.

Wakati tukielekea kwenye uzinduzi huo, ni vyema kutafakari maana, uzito na umuhimu wa dira hii.Si kama waraka wa serikali, bali kama kiapo cha taifa kwa vizazi vyake. Dira hii ni jicho la mbele la Tanzania, ikitazama mbali zaidi ya upeo wa leo, ikiwaalika wananchi wote kushiriki katika kuunda mustakabali wa pamoja.

Maana ya Dira ni sauti ya leo kwa ajili ya kesho, katika muktadha wa kitaifa, dira ni taswira ya nchi tunayoitaka kufikia katika kipindi maalum cha muda mrefu. Si tu maono ya maendeleo, bali ni mwelekeo unaounganisha ndoto zetu, dhamira zetu na juhudi zetu kama taifa moja. Ni mwanga wa mbali unaotuongoza kupitia giza la changamoto, kutuelekeza kwenye matumaini yaliyo makini.

Dira ya Taifa ya 2050 inajibu maswali ya msingi ambayo kila taifa lenye maono hujiuliza: Tanzania tunayoitaka ni ipi? Tunaamini katika misingi ipi ya utu, usawa, haki na maendeleo? Na ni hatua gani tunazopaswa kuchukua leo ili tufikie kesho bora zaidi kwa wote?

Tukumbuke dira ya wote, si ya serikali pekee. Ni muhimu kufahamu kuwa dira hii si mali ya serikali wala chama cho chote cha siasa. Ni zao la mazungumzo ya kitaifa, yaliyowahusisha wadau kutoka makundi mbalimbali ya jamii kama vijana, wanawake, wazee, walemavu, wakulima, wafanyakazi, sekta binafsi, viongozi wa dini, vyama vya siasa, wasomi na wananchi wa kawaida.

Ushirikishwaji huu wa kitaifa ni ishara ya ukomavu wa kisiasa na kijamii, lakini pia ni msingi wa uhalali wa dira hii mbele ya dhamira ya taifa. Kwa pamoja, kama taifa, tumekubaliana juu ya malengo ya msingi tunayoyahitaji licha ya tofauti zetu katika njia za kuyafikia. Tunatofautiana kwa sababu tunafikiri; lakini tunakubaliana kwa sababu tuna nia njema kwa taifa letu.

Na ni kweli kwamba tunaweza kutofautiana katika fikra na mitazamo. Hilo si kasoro wala udhaifu. Kutokukubali kuwa tuko tofauti ndio kasoro na udhaifu wenyewe. Mkono hutusaidia katika kazi zetu; lakini vidole vya mkono huo huo havilingani. Hata hivyo, vyote hufanya kazi kwa pamoja.

 Kasoro ya ufupi au urefu wa kidole hauondoi umuhimu wake kuwa sehemu ya mkono. Tusitafute usawa wa fikra au mitazamo bali tukubaliane kwamba sote tupo tofauti kwa faida ya wote. Muhimu zaidi, tukubali kutofautiana katika fikra na mitazamo; lakini tubaki kuwa wamoja.

Dira kama mwongozo wa taifa, katika mazingira ya ushindani wa kimataifa, changamoto za mabadiliko ya tabianchi, teknolojia, siasa na uchumi, taifa lisilo na dira ni sawa na meli isiyo na dira ya baharini. Dira ya Taifa ya 2050 inatoa mwongozo wa pamoja wa sera, mipango na utekelezaji kwa serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia, jamii na mtu mmoja mmoja.

Inapanga vipaumbele vya kitaifa kwa muktadha wa muda mrefu, inahamasisha mshikamano wa maendeleo, na inajenga utaratibu wa uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi wao. Dira huifanya Tanzania kuwa mahali pa matumaini kwa ndani na pa mvuto kwa wale wanaotafuta fursa ya kushirikiana nasi katika safari ya maendeleo.

La muhimu Tanzania mpya haijengwi kwa ndoto pekee.Dira haitoshi kwa maandishi. Inahitaji hatua. Na hatua ya kwanza ni kuielewa, kuimiliki na kuitekeleza kwa dhati. Tanzania mpya tunayoiota haijengwi kwa ndoto pekee bali kwa mikakati, mshikamano na nidhamu ya utekelezaji.

Ni wajibu wa kila Mtanzania kujitazama katika kioo cha dira hii na kujiuliza:

Ninachangia vipi katika kuiwasha taa ya mbele ya taifa letu?

Ninasimamia vipi malengo ya pamoja, huku nikiheshimu tofauti za fikra?

Watanzania wito kwa wote,  uzinduzi wa Dira ya Taifa ya 2050 ni zaidi ya tukio la kisera  ni mwaliko wa taifa kwa watu wake, wa kizazi hiki kwa vizazi vijavyo. Ni sauti ya leo inayoitikia kilio cha kesho. Ni msingi wa matumaini, dira ya mabadiliko, na kiapo cha kitaifa: kwamba hatutawaachia watoto wetu taifa bila mwelekeo.

Kwa pamoja, tuinue juu malengo ya taifa letu. Tuthamini tofauti zetu si kama kikwazo, bali kama utajiri wa fikra unaoimarisha msingi wa taifa jumuishi. Tuyakumbatie matumaini kama urithi wa pamoja matumaini yasiyojengwa juu ya hisia pekee, bali juu ya dira, mshikamano na hatua thabiti.

Na tuamke  kama kizazi kilichochagua kuandika historia yake kwa wino wa maridhiano, maarifa na ujasiri. Kwa dira ya pamoja, Tanzania inajenga kesho yake leo  kati ya ndoto ya wengi, na hatua ya kila mmoja.

Maoni: +1 437 431 6747