MWALIMU Julius Nyerere, Baba wa Taifa, aliipenda mno Tanzania, mwasisi na mdau mkuu wa Muungano wa Tanzania na Zanzibar.
Ni miongoni mwa wa wakuu wa nchi wachache wasiokuwa na makuu. Nyerere alikuwa mjamaa na asiyependa maisha makubwa, wanaomfahamu kwa undani wanasema alikuwa wa kawaida mno, akivaa suti za rangi ya kijivu muda mwingi.
Ni kiongozi ambaye hakupenda chochote cha bei mbaya, hakuwa muumini wa tafrija au sherehe kubwa, alikuwa akivaa kofia zikiwamo baraghashia. Hakuishi kwenye makazi au nyumba za gharama kubwa lakini pia kujistarehesha wakati watu wengi wanaishi kwenye hali ngumu.
Akizaliwa Aprili 13, 1922 katika familia ya Mzee Burito huko Mwitongo Butiama, alifariki akiwa na umri wa miaka 77 Oktoba 14, 1999 akipatiwa matibabu nchini Uingereza.
Mara nyingi, wasomi, wanasiasa, wachambuzi wa masuala ya uongozi, wanamrejea Mwalimu Julius Nyerere kama mfano wa mtu aliyeishi kwa ukamilifu na utimilifu asiyekuwa na tamaa ya mali, umaarufu wala kujilimbikizia utajiri, akiamini kuwa kufanya hivyo si sahihi, kwa sababu watu wengi aliokuwa anawaongoza walikuwa wakishindia maji, vipande vya miwa au hata tunda liwe chungwa, embe au ndizi.
Tanzania inapomsherehekea na kumbukizi za Baba wa Taifa, jina Mwalimu linaakisi mapenzi yake kwenye elimu Nyerere ni baba wa elimu, aliwekeza kwa kiasi kikubwa katika elimu ya watanzania na wakati wa uongozi wake uwezo wa kusoma na kuandika ulipanda, kwa asilimia 83 ya Tanzania wakijua kwa ufasaha kusoma na kuandika.
Mathalani, ripoti za Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO), zinaeleza kuwa kiwango cha watu wazima waliokuwa hawajui kusoma na kuandika kilipungua baada ya Uhuru 1961 na Azimio la Arusha, kutokana na kampeni kubwa za kuwahamasisha kujua kusoma na kuandika, ikiwamo ile elimu ya watu wazima na Elimu kwa Wote (Universala Pimary Education UPE), ikiishuhudia kupungua kwa kiasi kikubwa cha mbumbumbu wazee, vijana na watoto mijini na vijijini.
Kazi ya Nyerere iliigusa UNESCO, ikishangilia matunda yake kuwa ni taifa la kuigwa kwenye mafanikio kielimu.
Wakati takwimu za sasa duniani zinaonesha kuwa kusoma na kuandika bado ni ndoto kwa watu milioni 739 licha ya juhudi zinazoendelea kufanywa na mataifa kutokomeza hali hiyo.
Kadhalika hapa nchini, inakadiriwa kwamba watanzania milioni 11.59 hawajui kusoma wala kuandika. Serikali na wadau hawajapoa juhudi za kupunguza changamoto hiyo, zinafanywa usiku na mchana, kwa imani kuwa Tanzania bila wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK), inawezekana.
Taarifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, inaonesha kwamba asilimia 83 ya Wwatanzania 68,153,004 wanaojua kusoma na kuandika; ikiwa ni ongezeko la asilimia la 6.3 kutoka asilimia 78.1 wakati wa sensa ya 2012.
Tanzania inaendelea kufanyakazi ya Nyerere kuinua elimu ya wananchi mijini na vijijini, mathalani, taarifa za serikali zinaonesha kwamba, ili kufikia lengo la watanzania wote kujua KKK ni lazima kutekeleza afua mbalimbali, ikiwamo kuondoa vikwazo vya kupata elimu kama vile kutolewa kwa elimu ya msingi hadi sekondari bila ada na elimu ya lazima kuwa ya miaka 10.
Nyingine ni kutekeleza programu zenye lengo la kuwafikia watanzania waliokosa fursa za elimu kwa mfumo wa elimu ya watu wazima na ujifunzaji endelevu, utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kisomo pamoja na kutoa fursa kwa wanafunzi walioacha masomo, kwa sababu mbalimbali kurudi shuleni na kuendelea na masomo (re-entry program), kupitia Waraka Namba 2 wa Mwaka 2021.
Kadhalika, serikali imeendelea kuboresha huduma za maktaba nchini katika ngazi za mikoa, wilaya na shule ikiwa ni pamoja na maktaba mtandao, ili kuwawezesha watanzania wengi zaidi katika maeneo mbalimbali kupata huduma ya kujisomea popote waliko.
Aidha, serikali ya awamu ya sita inaendelea kumuenzi Nyerere ikiboresha mitaala, mazingira ya kufundishia, miundombinu, kuongeza ujuzi na teknolojia kwa walimu, kusogeza kampasi za vyuo vikuu mikoani, kujenga vyuo vya ufundi (VETA) wilayani na mikoani na kuboresha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, lengo ni kuongeza fursa kwa watanzania wengi zaidi kupata elimu bila kujali umri wala mazingira.
Taasisi hiyo imeundwa kwa lengo mahsusi ya kuwezesha vijana na watu wazima pamoja na makundi mengine ndani ya jamii, kupata elimu, stadi za kazi, ujuzi na maarifa, ili zitumike kama chachu na nyenzo muhimu kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha.
Pia, serikali inawekeza ili kusiwe na wananchi wasiokuwa na ujuzi, stadi nyenzo na maarifa ya kutosha, taifa liwe na nguvu kazi stahiki kwa maendeleo ya jamii, kuwezesha kila raia kuwa na uwezo, fursa na shauku ya kushiriki moja kwa moja katika harakati za uanzishwaji wa miradi ya maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii.
UNESCO linasema kuwa kujua kusoma, kuandika na kuhesbu ni haki ya msingi ya binadamu kwa kuwa ndiko kunakofungua mlango wa kufurahia haki nyingine za binadamu, uhuru mpana zaidi na uraia wa kimataifa.
UNESCO kama alivyokuwa Nyerere na hata sasa serikali kwa pamoja msisitizo wao ni kuwa na elimu na maarifa ni msingi unaowezesha watu kupata maarifa mapana zaidi, stadi, ujuzi, maadili, mitazamo na tabia zinazochochea utamaduni wa amani ya kudumu unaojengwa juu ya kuheshimu usawa, kutokubaguana, utawala wa sheria, mshikamano, haki, utofauti na uvumilivu na pia katika kujenga mahusiano ya maelewano baina ya mtu na nafsi yake, watu wengine na dunia pia.
Juhudi za kuwaelimisha wananchi ni tofauti kama ilivyokuwa enzi za Nyerere, leo uwapo wa zana za kidijitali umewezesha kupanua fursa za kujifunza na kufundisha kwa raia wote yakiwamo makundi yaliyotengwa, wakiwamo wenye mahitaji maalumu wanaofunzwa kupitia programu za elimu jumuishi, wazee, wana kaya maskini ambao mabadiliko ya kidijitali yanawatengenezea fursa za zaidi za kujifunza kusoma na kuandika na pia kupata mafunzo kupitia taasisi kama VETA.
Taifa linapomkumbuka Mwalimu wadau waendelee kushirikiana na serikali kufanikisha juhudi za kupata elimu bora na kuwezesha kila raia kujua KKK, kupata na kutumia maarifa kuanzia ya maarifa asilia hadi ya kidijitali yanayopatikana duniani leo, ambayo ni nyenzo muhimu ya kufanya mabadiliko ya kuchumi na kijamii, kwa njia salama na zinazofaa bila gharama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED