ANVER Versi, ni mwandishi wa habari. Mzaliwa wa Kenya, ambaye kwa sasa anaishi nchini Uingereza. Huyu ni mwanafunzi wa mwanafasihi nguli, Ngũgĩ wa Thiong’o.
Versi, alikuwa mmoja wa wanafunzi wake katika miaka ya 1970.
Ana simulizi kumhusu Ngũgĩ wa Thiong’o, mwandishi aliyebobea kwenye sanaa hiyo, ameaga dunia mwishoni mwa wiki, huko Marekani, akiwa na umri wa miaka 87.
Katika andiko lake, alilolitoa Juni 2, mwaka huu, kwenye jarida la New African, Versi anamwelezea Ngũgĩ, kama mwalimu, ambaye hakuwa na woga na mwanaharakati wa haki za binadamu.
Anamtaja Ngũgĩ, mtetezi jasiri wa haki za watu katika mapambano yao dhidi ya ukandamizaji, aliyeandika fasihi pia kwa lugha za Kiafrika.
“Nilikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Nairobi mwanzoni mwa miaka ya 1970 na Ngũgĩ wa Thiong’o alikuwa mhadhiri wangu wa Fasihi ya Kiafrika.
Fasihi ilikuwa somo nililolipenda sana tangu nikiwa shule. Nilifurahia kusoma kila kitabu nilichoweza kukipata na kulikuwa na vyanzo viwili vya furaha yangu hiyo.
Kimoja kilikuwa Maktaba ya British Council huko Mombasa, na kingine kilikuwa duka dogo la vitabu vya mkononi linaloendeshwa na mzee mmoja aliyezoea kuniruhusu nichukue vitabu bila kulipa.
Ingawa mandhari yalikuwa mageni na magumu kuyaelewa, kwani nilizoea tu jua kali au mvua za ‘monsoon’ hisia za wahusika wa hadithi hizo zilikuwa za kawaida na nilizielewa.
Lakini pia nilijaza kiu yangu ya hadithi kupitia Mama Andikalo, ambaye alitekwa utotoni na kuuzwa utumwani kabla ya kuokolewa na babu yangu upande wa mama kule Zanzibar.
Alituambia hadithi za Kiswahili zilizodumu kwa wiki nzima. Hadithi zake zilihusu wahusika kama akina Ali na Masoodi, au Mamadi Mkula Guniya aliyekuwa na nguvu za ajabu (Juma ambaye angeweza kula gunia zima la mchele kwa kikao kimoja).
Pia, Mamiya Ndege aliyekuwa mtawala wa dunia ya ndege; na Jamila ambaye uzuri wake uliwafanya samaki waruke baharini walipoona picha yake, na kujikuta wakigeuka kitoweo.
Kando na hayo, kulikuwa na sinema za Kihindi zilizojaa mapenzi na misukosuko, zilizopendwa na watu wa rangi zote na simulizi za yaliyotokea kwenye filamu hizo ambazo zilirejewa mara kwa mara. Hivyo basi, tulishiba hadithi za aina mbalimbali kwa lugha tofauti.
Hata hivyo, vitabu vya shule vilijikita tu kwa waandishi wa Kiingereza kama Shakespeare, Charles Dickens, George Eliot, Joseph Conrad, Jane Austen na wengineo.
Hakukuwa na kazi za waandishi wa Kiafrika, hivyo tulidhani Waafrika hawaandiki vitabu, japokuwa tulijua kuwa walikuwa waandishi hodari wa hadithi kwa mdomo.
Utambulisho wangu wa kwanza rasmi kwa fasihi ya Kiafrika ulitokea nilipokuwa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Nairobi.
Wakati huo, Idara ya Fasihi ya Kiingereza ilikuwa imebadilishwa jina kuwa Idara ya Fasihi tu na Fasihi ya Kiafrika, ikawekwa katikati ya mtaala.
Baadaye, niligundua kuwa aliyesukuma mabadiliko haya alikuwa Ngũgĩ wa Thiong’o.
Wakati huo, waandishi wachache sana wa Kiafrika walikuwa wamechapishwa, hasa kupitia mfululizo mzuri wa vitabu vya Heinemann African Writers Series, ambao kwa mara ya kwanza walichapisha ‘Things Fall Apart’ ya Chinua Achebe mwaka 1958.
Waandishi wa Afrika Magharibi kama Achebe na mwenzake kutoka Nigeria, Wole Soyinka, walikuwa tayari wamejipatia heshima kama waasisi wa aina hii mpya ya fasihi.
Katika Afrika Mashariki, tulikuwa na Ngũgĩ wa Thiong’o, ambaye hapo awali alijulikana kama James Ngugi, riwaya yake ya kwanza, ‘Weep Not, Child (1964)’, ilifuatiwa haraka na ‘The River Between (1965)’ na ‘A Grain of Wheat (1967).”
Versi, anasema wakati huo vitabu vya mtaala katika orodha za kusoma wakati huo vilitawaliwa na waandishi wa Kiingereza na Kimarekani.
“Kama kumbukumbu zangu ni sahihi, nakumbuka waandishi kama Jane Austen na John Steinbeck (The Grapes of Wrath, Of Mice and Men), pamoja na mashujaa wengine wa fasihi ya Kiingereza.
Kitabu cha Achebe, ‘Arrow of God’, kilikuwa miongoni mwa vitabu vya lazima katika sehemu ya fasihi ya Kiafrika, ambayo ilikuwa nyembamba sana kwa wakati huo.
Nakumbuka msisimko mkubwa uliozuka tulipoambiwa kuwa Ngũgĩ ndiye angekuwa mhadhiri wetu kwenye ‘Arrow of God’. Ukumbi wa mihadhara ulijaa watu waliokuwa wakimsubiri kwa hamu.
Alipoingia, alifanya hivyo kwa unyenyekevu mkubwa, na wengi wetu tulishangazwa kidogo kuona kuwa alikuwa mfupi wa kimo. Kwa sababu fulani, tulikuwa tumemfikiria kuwa mtu mrefu au mwenye umbo kubwa, kwa nini? Hatujui.
Wahadhiri wengine wa fasihi, hasa Waingereza na Wamarekani, walikuwa watu wa maigizo, waliopenda maonesho na wenye ushawishi wa kisanaa.
Walitufanya kucheka sana walipokuwa wakichambua vichekesho vya kijamii vya Jane Austen au walipotufanya tuvutiwe kabisa walipozungumzia matumizi ya ishara na tamathali ya lugha katika ‘Heart of Darkness’ ya Conrad.
Ngũgĩ, kwa upande mwingine, aliepuka kwa makusudi maonesho ya kihisia au mbwembwe yoyote. Mara ya kwanza tulipomwona, alikuwa amevaa shati lisilo na tai na koti la corduroy lenye rangi ya vumbi.
Bila kupoteza muda, alianza kazi kwa sauti ya chini sana, kama mnong’ono.
Ilikuwa vigumu sana kufuata mhadhara wake kwa sababu mara nyingi alielekea katika maeneo magumu kuyaelewa, kwa mfano, alijikita katika uchambuzi wa ishara za kidini na kitamaduni katika kazi ya Achebe.
Wakati mwingine alitumia nusu ya mhadhara, au hata mhadhara mzima, kuchambua aya moja au mbili pekee katika ‘Arrow of God’, akieleza mpangilio wa sentensi na kwa nini kila neno lilikuwa mahali pake hasa.
Tulihisi kana kwamba tulikuwa tukipewa almasi za kiakili ambazo akili zetu hazikuwa tayari kuzishika. Alama zetu katika insha zilikuwa chini sana, isipokuwa kwa Lars (kama nakumbuka vizuri), ambaye alitoka Finland na alikuwa akisoma chuoni kwetu kwa sababu baba yake alikuwa balozi.
Alama zake zilikuwa mara mbili ya aliyefanya vizuri zaidi kati yetu.
Siku moja, Lars, ambaye alikuwa rafiki yangu wa karibu, aliniita pembeni na kunionesha siri ya mafanikio yake.
Alikuwa na kinasa sauti na alikuwa akinasa mihadhara yote ya Ngũgĩ badala ya kujaribu kuandika kila kitu kwa haraka kama sisi wengine.
Aliweza kumsikiliza Ngũgĩ kwa utulivu kwa marudio. Tangu wakati huo, nilianza kufanya kazi kwa kutumia rekodi hizo na alama zangu darasani zilipanda sana.
Wakati mwingine, Ngũgĩ alijiunga nasi kwenye ‘Junior Common Room’ na kikombe cha chai na vitafunwa.
Tukiona alikuwa katika hali nzuri ya moyo, mimi na rafiki yangu Mfinland tulimwomba tuketi naye mezani.
Katika nyakati hizo, alikuwa mtu tofauti kabisa. Alikuwa ametulia, akizungumza mchanganyiko wa Kiingereza na Kiswahili na akionesha ucheshi wa hali ya juu na akili ya haraka.”
MGONGANO USIOEPUKIKA
“Bila sisi kujua, kulikuwa na mikondo ya chini iliyokuwa ikivuma. Riwaya zake tatu za mwanzo zililenga mahusiano kati ya watawala wa kikoloni na wakulima wa Kenya, wengi wao wakiwa wameporwa ardhi na kuishia kuwa vibarua kwa ujira mdogo kwenye mashamba ya wakoloni.
Katika kitabu ‘A Grain of Wheat’, aliunda simulizi yenye mvutano mkubwa juu ya mvutano kati ya mapambano ya ukombozi na hamu ya kuishi, hata kama ni kwa kumsaliti yule unayempenda zaidi.
Lakini mwelekeo wake uligeuka kabisa alipokiandika ‘Petals of Blood’ mwaka 1977. Riwaya hiyo iliangazia kipindi cha baada ya ukoloni.
Alikuwa na imani kuwa watu waliolipa gharama ya uhuru kwa maisha yao walikuwa wamehujumiwa na kwamba tabaka jipya la Waafrika wenye fedha na madaraka walikuwa wamechukua nafasi ya wakoloni Wazungu, lakini hawakujali kabisa kuhusu maslahi ya watu wa kawaida. Huu ulikuwa usaliti mkubwa.
Carey Baraka, mwandishi wa Kenya aliyemtembelea Ngũgĩ akiwa mgonjwa karibu mwaka mmoja kabla ya kifo chake nyumbani kwake mjini Irvine, Marekani, alipokuwa profesa wa fasihi linganishi katika Chuo Kikuu cha California, aliandika:
“Akiwa amevutiwa sana na maandiko ya Karl Marx na Frantz Fanon, katika kazi zake za baadaye Ngũgĩ alianza kujikita moja kwa moja na masuala ya dola, tabaka, elimu, na vipengele vyote vya maisha baada ya ukoloni.
‘Petals of Blood’, iliyochapishwa mwaka 1977, ilishambulia tabaka la kisiasa la Kenya huru.
Hii ilikuwa riwaya ya kwanza aliyoandika kwa kutumia jina la Ngũgĩ wa Thiong’o na ya mwisho aliyoandika kwa Kiingereza.”
“Katika riwaya hii, elimu haikuwa tena chombo cha ukombozi; waliosoma waligeuka kuwa wasaliti wa watu. Hili lilikuwa shambulio la kwanza kutoka kwa yule ambaye mkosoaji Nikil Saval alimwita ‘Ngũgĩ wa kipindi cha hasira, aliyechoma hadharani tabaka la mabepari wa Kenya waliobeba vijiti vya gofu na kurudia maisha ya kikoloni waliyokuwa wameyakataa hapo awali’.”
TOFAUTI NA WAFASIHI WENGINE
“Pengine kilichomtofautisha sana Ngũgĩ na waandishi wenzake ilikuwa ni msimamo wake thabiti wa kukataa kabisa lugha ya Kiingereza.
Wakati waandishi wengi walikiona Kiingereza kama chombo cha kuwaunganisha watu na kufikisha ujumbe kwa hadhira pana, Ngũgĩ aliamini kuwa haiwezekani kuondokana na fikra za kikoloni, iwapo mtu ataendelea kuandika kwa lugha ya mkoloni.
Katika kitabu chake maarufu ‘Decolonising the Mind’, alikosoa kwa nguvu athari za lugha za kikoloni kama Kifaransa na Kiingereza katika nchi zilizowahi kutawaliwa.
Msimamo wake huu kuhusu matumizi ya lugha uliwahi kuleta mivutano kati yake na Chinua Achebe, ambaye alimhifadhi na kumshika mkono mwanzoni hadi kuingizwa kwenye mfululizo wa ‘African Writers Series’. Mjadala huo kuhusu lugha unaendelea hadi leo.
“Kwa mtazamo wangu binafsi, najihisi mwenye bahati kuwa mwanafunzi wa mmoja wa mashujaa wangu wa fasihi. Sasa ninatambua kina cha uelewa wake.
Si tu wa fasihi ya Kiafrika, bali pia wa urithi mpana wa kiutamaduni wa bara hili unaonyoosha hadi milenia nyingi. Alinichukua katika safari ambayo hadi leo haijafikia tamati na alinifundisha kuthamini hadithi zote, kwa lugha zao zote, zilizonisindikiza tangu utotoni.
Kwamba gwiji huyu wa fasihi ya dunia, ambaye mara nyingi alitarajiwa kushinda Tuzo ya Nobel, hakuwahi kutuzwa ni miongoni mwa mifano ya wazi kabisa ya dhuluma katika historia ya tuzo hiyo.
“Lakini urithi wake utaishi milele. Bado ninaweza kumuona akiwa amesimama ukumbini, tabasamu dogo usoni, macho yake yenye mvuto na upole yakianza kutufunua mafumbo ya riwaya ya Kiafrika na kicheko cha chinichini kilichotokea machoni mwake, kila alipotoa utani kwenye Junior Common Room ya chuo kikuu, tukiwa tunakunywa chai iliyotengenezwa kwa majani kutoka sehemu aliyopenda zaidi ya nchi yake.
Pumzika kwa amani, Ngũgĩ wa Thiong’o, vita uliyoiwasha ya kutafuta haki bado inaendelea.”
NEW AFRICAN
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED