NYERERE 1922-1999; Aliamini elimu bora ya Mtanzania ndiyo mlango maendeleo ya taifa

By Salome Kitomari , Nipashe
Published at 05:32 PM Oct 15 2025
Mwalimu Julkius Nyerere
Picha: Mtandao
Mwalimu Julkius Nyerere

TAIFA linaendelea na kumbukizi ya Mwalimu Julius Nyerere ambaye mwaka 1970, akizindua Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mambo aliyosisitiza kwenye sekta ya elimu ni umuhimu wa uhuru na wajibu wa kitaaluma na kunoa nguvukazi ikifanikisha maendeleo.

Hata baada ya miaka 55 hotuba hiyo inaishi hasa katika wakati ambao  taifa lolote ili liendelee linahitaji nguvukazi iliyoelimika inayoweza kuzalisha na kukuza uchumi wake kutumia ubunifu, uvumbuzi na maarifa mapya.

Katika Chuo Kikuu Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki linafanyika Kongamano la Kumbukizi ya Mwalimu Nyerere linaloandaliwa na kusimamiwa na Kigoda cha Uprofesa cha Mwalimu Julius Nyerere katika taaluma za umajumuni wa Afrika cha UDSM kwa ushirikiano na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na  Binafsi (PPPC), likiwaleta pamoja wadau mbalimbali kujadili suala la uchumi jumuishi.

Miongoni mwa watoa mada ni Mkurugenzi Mtendaji wa PPPC, David Kafulila, anayesema katika kujenga uchumi shindani ushirikiano na sekta binafsi ni suluhisho la changamoto za kijamii na kwamba lengo ni kuihusisha ili  itoe mchango wa mitaji, teknolojia na ufanisi kufikia Dira 2050 inayolenga kujenga uchumi wa Dola trilioni moja.

“Kituo cha ubia na dhana ya ubia ni njia muhimu ya kufikia Dira 2050, itakumbukwa Mwalimu Nyerere alisisitiza ubia uanze na wawekezaji waliopo ndani wenye mtaji, si dhana ngeni na fikra muhimu kujenga uchumi, changamoto yake watu wanachanganya kati ya ubia na ubinafsishaji. Ubia ni ndoa kati ya serikali na umma, umiliki ni mali ya umma, kabla, wakati na baada, kinachotokea ni kugawanya vihatarishi kati ya serikali na mwekezaji,” anasema.

Kwa mujibu wa Kafulila, mwaka 1968 Mwalimu Nyerere alihutubia Chuo Kikuu cha Liberia, alipozungumzia umuhimu wa wajibu wa kitaaluma na uhuru wa kitaaluma, huku akimfananisha mwanafunzi wa chuo kikuu na trekta kwa mkulima linalonunuliwa kuongeza tija kwenye kilimo, hivyo mwanafunzi ana thamani ya elimu yake kwenye uzalishaji, kujenga uchumi na kuleta maendeleo ya taifa.

“Ni muda wa kutafakari mawazo ya Nyerere kuhusu mwanafunzi wa chuo kikuu kuwa kama trekta kwenye uchumi wa nchi bado ni sahihi na kwa kiasi gani ni sahihi? Tangu Mwalimu Nyerere azungumze  miaka 57 imepita lakini kauli yake imebaki kuwa ukweli wa dunia kwamba kwa kiasi gani nguvu kazi inachangia ukubwa wa uchumi, dunia ya leo umbali kiasi gani unakwenda inategemea ubora wa nguvu kazi uliyonayo.”

Kafulila anasema Jarida la Oxford la Aprili 2014, lilionesha katika mataifa 13 makubwa kiuchumi  duniani asilimia 62 ya utajiri wao umetokana na nguvu kazi, asilimia 25 ufanisi wa kitaasisi huku asilimia tano ikiwa ni maliasili.

“Nguvu kazi yenye ubora ina thamani kubwa kwenye kujenga uchumi kuliko maliasili, na kwamba kuna mataifa yana maliasili nyingi lakini ni maskini na yapo hayana maliasili maskini pia, na yapo yasiyo na maliasili na ni tajiri na yenye maliasili na matajiri na  kwamba kwa mlingano huo sababu ya msingi ya utajiri wa taifa ni ubora wa nguvu kazi,”anaeleza.

Anakumbusha kuwa Chuo Kikuu Dar es Salaam kiliunda nadharia ya fikra za Dar es Salaam kwa mtangamano wa  fikra kuhusu Afrika, heshima  iliyojengwa miaka mingi, ambayo imekuwa fikra za Tanzania ndiyo maana Mwalimu Nyerere alipozungumza na wazee wa Dar es Salaam aliaamini  amezungumza na taifa zima.

 “Nguvu kazi inatumika kuelezea uchumi wa nchi ikiwamo Tanzania ambayo imewekeza kwenye rasilimali watu hadi tulikofika, kama taifa tumeendelea ni  kwa kiasi gani ni mjadala, wakati Rais  Samia Suluhu Hassan, anaingia madarakani kiasi kilichotumika kwenye elimu kilikuwa Dola 105 na sasa ni 150, kwenye afya ilikuwa Dola 36 na sasa 55,” anafafanua.

Anaeleza kuwa kwenye nguvu kazi unapima kwa kuangalia lishe, maarifa na afya na kwamba uamuzi wa kuwekeza kwenye maeneo hayo umeongeza umri wa kuishi na kwamba mawazo ya Mwalimu Nyerere yametimia, kwa kuwa hakuna namna ya kufika mbali bila kuwekeza kwenye nguvukazi,  ndiyo maana kwenye Dira 2050 wamegusa eleza.

Aidha, anatoa mfano wa China kwamba ilikuwa nyuma sana lakini iliwekeza kwenye nguvukazi yenye ubora, na kwamba mitaji mingi kutoka Marekani na Ulaya ilikwenda China kwasababu alikuwa na nguvu kazi, uzalishaji nafuu unaoleta faida.

“Tunapotaka kuvuta mitaji kutoka sekta binafsi ya ndani na nje, jambo linaloamua ni nguvu kazi tuliyonayo ina maarifa kiasi gani, mwekezaji anaweza kushindwa kuwekeza nchi fulani kwasababu wataalamu anaowataka hawapo.Tunapofikiria uchumi wa Dola trilioni moja kama Dira 2050 ionayosema ni lazima kuwekeza kwenye nguvu kazi.

Mkurugenzi huyo anasema uamuzi wa kufanya mabadiliko ya mitaala ya elimu ni ili nchi iwe na nguvukazi yenye ubora kwa kuwa tayari inaonesha kati ya asilimia 30 hadi 35 kuna ajira zinakosa wataalam wenye taaluma mahususi na kuwalazimisha kuchukua kutoka nje ndiyo maana ni muhimu kuboresha elimu.

Aidha, anasema uchumi wa dunia haupimwi kwa idadi ya watu kwenye nchi au bara bali kwa ubora, na kwamba Ulaya ina watu asilimia saba ya dunia, inamiliki asilimia 25 ya uchumi duniani, lakini Afrika bado ni changamoto kwasababu ya uduni wa nguvu kazi iliyopo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, akishiriki kongamano anasema  Tanzania ni nchi ya watoto na vijana hivyo lazima uwekezeji ulenge kundi hilo.

“Maana yake ni hii ukiwa na watu wengi wadogo mipango yako lazima ielekee kwenye elimu, ukiwa na wazee wengi uwekezaji mkubwa ni kwenye afya, hii inatutaka lazima tuwekeze kwenye elimu ili taifa liendelee, Simu na intanet imekuwa nyezo ya kujifunza, ya kusaka na kusambaza maarifa ambayo vijana wanapaswa kuitumia vyema,” anaongeza.

Kwa mujibu wa Prof. Kitila, Mwalimu Nyerere anasema silaha tuliyonayo ni elimu, na kwamba ukubwa, uzito na uimara wa taifa si kuwa na majeshi na silaha kiasi gani bali watu wako wana elimu kiasi gani, na kwamba utake usitake elimu ni silaha muhimu kupambana na chochote ikiwamo kujenga uchumi na ndio maana Dira 2050 imeipa kipaumbele.

Mkurugenzi  Mtendaji wa Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara (TWCC), Dk. Mwajuma Hamza, anasema hofu ya sekta binafsi ni kuwajengea uwezo waajiriwa ambao baada ya muda wanaondoka na kushauri kuwepo uwezeshaji kwa sekta binafsi.

“Tunalipa kodi ya huduma lakini muda mrefu tunaomba irudi kusaidia sekta binafsi kuwajengea uwezo na kwamba katika kutekeleza Dira 2050 ni muhimu suala hilo likaangaliwa. Nguvu kazi bora haijengwi bila elimu bora tunapongeza serikali kwa kuhakikisha kila mtoto anamaliza shule.”

Aidha, anasema utafiti wa mwaka 2023 wa sekta binafsi umebaini kuwa zaidi ya asiimia 80 ya wahitimu hawana sifa zinazotakiwa kwa kuwa sekta binafsi kila kitu kinaangalia biashara, hivyo wanatazama aina ya watu wengi.

“Tuna biashara nyingi hapa Tanzania ila hakuna nguvukazi ya kufundisha nguvukazi mpya inayotoka vyuoni, sekta binafsi tunatamani kupata watu ambao wako tayari, vyuo vitusaidie wahitimu wawe bora kukidhi matakwa ya ajira.Zamani UDSM ilisaidia sekta binafsi  ilisaidia waajiri binafsi kupata watu bora si wapya wa kufundisha,”anaoneza Mwajuma.

“Baadhi ya nchi zimekuja na mfumo shirikishi kati ya sekta binafsi, serikali na nyuo vya elimu kwamba kabla ya kuanzisha kozi lazima kuangalia soko linataka nini, hivyo wawekeze kwenye utafiti wenye kuleta suluhu ili kusaidia kupata nguvukazi bora, wanafunzi kabla hawajamaliza wanajua wanakwenda kufanyakazi wapi,”anasisitiza. 

Dk. Mwajuma anasema kuelekea kutekeleza Dira 2050 kuweka vivutio vya kikodi kwa kampuni zinazotengeneza watu, na kwamba kama hakuna biashara nyingi zitakuwa na woga kwa kuwa sekta binafsi inaangalia pesa, matokeo na uwekezaji, pia kuanzia mfuko wa taifa wa uwekezaji na ujuzi ili kusaidia kujenga nguvu kazi.

Kufanya mfumo wa nguvukazi ambao usajili wa kanzi data ya mafunzo na ujuzi kwa vitendo ili kutambua ambao hawajaariwa na uwezo wao, na kwmaba nchi nyingi hupenda kuangalia nguvukazi na ujuzi uliopo, na kwamba kwasasa zipo lakini hazihawekwa vizuri.

Aidha, anasema ni muhimu kusisitiza usawa wa kijinsia kwenye ajira kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu kutoa mchango wao kwenye maendeleo ya nchi, na kuhakikisha kila kampuni iakuwa na sera ya kuhakikisha wanawake wanashiriki nafasi za uongozi.

“Nguvukazi yenye ujuzi si anasa bali ni hitaji la taifa, tuna Dira 2050 na Sera Mpya ya Elimu, sasa ni wajibu wa kutengeneza guvu kazi, Ujerumani anapewa mtihani na waajiri wa sekta binafsi maana ndiyo wanajua wanahitaji watu wenye sifa zipi,”anabainisha.

Akifungua kongamano hilo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, anasema serikali itaendelea kuhakikisha Tanzania inakuwa na nguvukazi yenye ujuzi wa kisasa na inayoweza kushindana katika soko la ajira la kikanda na kimataifa. 

Anasema lengo ni kuhakikisha nguvu kazi hiyo inakuwa na mchango katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

 “Mafanikio ya taifa letu katika miaka ijayo yatategemea kwa kiasi kikubwa ubora wa watu wake. Msingi wa maendeleo ni watu wenye ujuzi, ubunifu, na maadili. Tuweke mbele elimu bora, ujuzi, ubunifu, na uzalendo kama silaha za kujenga taifa lenye ustawi, amani na maendeleo jumuishi.

Anasema ili Tanzania iandae nguvu kazi imara kwa kuitekeleza mipango mbalimbali ikiwemo kuanzisha Programu za Elimu ya Ufundi na Ujuzi (VET na TVET) kwa kupanua wigo wa vyuo vya VETA katika kila wilaya na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopata mafunzo ya vitendo.

“Pia serikali imeanzisha Programu ya Taifa ya Maendeleo ya Ujuzi (National Skills Development Programme) inayolenga kujenga ujuzi kwa vijana katika sekta za kilimo, viwanda, teknolojia, nishati na huduma”, akitoa  wito kwa vyuo vikuu, taasisi za utafiti, sekta binafsi, na vijana kushirikiana katika kutekeleza kwa vitendo malengo ya Dira ya Taifa 2050

Katika hatua nyingine, Majaliwa anatoa wito kwa taasisi za biashara, viwanda, na mashirika binafsi kwa kushirikiana na taasisi za serikali kuanzisha programu za mafunzo kwa vitendo kazini kukuza stadi za kazi.

Awali, Makamu Mkuu wa Chuo UDSM, Prof. William Anangisye anataja lengo la kongamano kuwa ni kutafakari, kuenzi na kuangazia urithi wa misingi ya fikra za Mwalimu Nyerere kwa kizazi cha sasa kwa mustakabali wa nchi.

Mada kuu ya kongamano hilo ni nguvu kazi yenye ujuzi kwa maendeleo ya taifa, kuendeleza urithi wa Mwalimu Nyerere kuelekea Dira 2050, na kwamba inaakisi dhamira ya dhati ya taifa ya kujenga jamii yenye maarifa, studi na uwezo wa kushindana katika karne ya 21, 

Prof. Anangisye anasema UDSM inatambua kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kutokea bila kuewekeza katika rasilimali watu, bila kuandaa kizazi cheye ujuzi, elimu ya maadili na uzalendo na kwamba ndiyo roho ya urithi wa Mwalimu Nyerere kuiamini kuwa ni  nyenzo ya ukombozi, ustawi na mshikamano wa kitaifa.