CHAMA cha ACT Wazalendo , kinaendelea kupeleka ujumbe kuwahamasisha wananchi kujitokeza kuchagua viongozi wanaowataka, pia kupiga na kuzilinda .
Viongozi wa chama hicho wakiwa kwenye makundi mawili moja likiongozwa na kiongozi mkuu wa Chama Dorothy Semu na jingine chini ya Zito Kabwe, kiongozi mkuu mstaafu wa chama hicho.
Kwa pamoja wanafikisha ujumbe kwa wananchi na kuwataka kupiga kura na kuzilinda wakiwa na kauli kuu isemayo 'Oktoba linda kura’, anasema Zitto akiwa Tunduru mkoani Ruvuma.
Anaeleza kuwa endapo chama hicho kikishika dola kitaweka utaratibu wa kisayansi ya kuvuna tembo Ili kuwapunguzia wananchi adha inayotokana na uharibifu kutokana na wanyama hao.
Anasema jambo jingine watakalo fanya ni kupitia upya mipaka ya hifadhi na kuwapa wananchi maeneo makubwa ya kufanya shughuli zao za kiuchumi.
"Tutavuna tembo, hivi sasa kila mahali tembo tembo...lakini kubwa kuliko zote na kuiondoa CCM madarakani," anasema Zitto ambaye ni mbunge wa zamani wa Kigoma Mijini.
Katika ziara hiyo anaeleza kushangazwa na hatua ya serikali kuzuia matumizi ya mkaa wakati gharama ya gesi ipo juu na bajeti ya mwaka huu haikuzungumzia jambo hilo.
Anashauri iondoe kodi lukuki kwenye gesi ili ishuke bei hata mwananchi wa kipato cha chini waimudu na kuitumia ili kutimiza azma ya kutunza mazingira.
Anasema nchi ina gesi nyingi lakini serikali ya CCM, inachelewa kuwekeza fedha zisizozidi Sh. bilion 100 kwa ajili ya kutengeneza mtambo unaochakata na kufungasha gesi asilia (LNG) kwa matumizi ya nyumbani.
Anasema kushindwa kutekeleza hilo kumefanya serikali inunue gesi kutoka nje ya nchi na kwamba kibaya zaidi wameweka katazo la matumizi ya mkaa bila kuwapo na nishati mbadala.
Anasema hicho ni kiashiria kwamba CCM imechoka na haipaswi kuendelea kuongoza nchi huku akiwasisitiza Wanaruvuma kukikataa chama hicho.
"ACT Wazalendo ingekuwa inaongoza serikali ingewekeza kwenye mtambo wa kufungasha gesi asilia ili bei iwe ndogo au kuwekeza katika teknolojia ya uzalishaji wa makaa ya mawe yanayochimbwa hapa kwenu," anasema Zitto.
ALIA NA USHURU
Mwanasiasa huyo, anasema iwapo chama chake kitaingia madarakani kitafuta ushuru wote katika mazao ili wakulima wanufaike na mazao yao.
Anasema sera ya serikali inasema ushuru hautakiwi uzidi asilimia tatu ya thamani ya zao lakini anashangazwa kuona wakulima wanatozwa zaidi ya kiwango hicho.
"CCM imeziacha halmashauri zinajiamulia ushuru iwe kiasi gani, ufuta ni zao kubwa nchini, dunia nzima inazalisha tani milioni sita za ufuta, sisi ni wa tano duniani kwa kuuza ufuta nje na ni wapili Afrika kwa kuzalisha zao hilo kwa wingi" anasema Zitto.
Anakumbusha faida za zao hilo kwamba mwaka jana pekee serikali iliingiza matrilioni ya fedha.
"Ushuru kwa wakulima bado wanalipa mkubwa, makaa ya mawe ushuru wake ni kiduchu lakini mahindi tani 30 ushuru Sh. 900,000 hizo ndio sera za CCM, matajiri wanalipa kidogo masikini zaidi," anadai Zitto.
Anasisitiza msimamo wake watakaposhika madaraka watafuta ushuru na wakiulizwa na watu wa CCM halmashauri zitaendeshwaje watawajibu chama hicho kina vijana wametafiti wamegundua ushuru wa mazao nchi nzima unakusanya Sh. bilioni 135 kwa mwaka sawa na asilimia nane ya mapato ya halmashauri zote nchini na hivyo zile zinazotegemea fedha hizo watazifidia kutoka hazina ili mkulima abaki na fedha ya kutosha.
INAKUWAJE CCM 99%?
Akiwa Moshi Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu anasema sababu inayowafanya kushiriki uchaguzi ni kwa sababu wananchi ndiyo wenye mamlaka ya kuiweka au kuiondoa serikali madarakani.
"Tunataka Mtanzania atambue kura yake ndiyo yenye uamuzi. Haiwezekani wao wapate asilimia 99 katika uchaguzi uliopita halafu sisi vyama vya upinzani vyote tuambulie asilimia moja?” Anahoji?
"Sisi sio watu wa kutetereka ni chama makini kinachojifunza kutokana na historia ya nchi mbalimbali mageuzi yoyote yaliyowahi kutokea duniani ni zao la mapambano.
"Hatutawapa CCM hiyo nafasi ya kubaki peke yako katika uchaguzi...atakavyo lala ng'ombe ndivyo atakavyo chinjwa na tunahakika tutakwenda kushinda" anasema Dorothy.
Anaitaka serikali kuhakikisha Sh.trilioni moja iliyotengwa kwa ajili ya uchaguzi inatumika kuimarisha demokrasia na sio kupoka uhuru wa watu kuchagua kiongozi wanayemtaka.
"Serikali imetenga bajeti ya trilioni moja kwaajili ya uchaguzi...tunaikumbusha fedha hizo zinatakiwa zitumike kuboresha na kulinda demokrasia hususani haki ya Watanzania kuchagua viongozi wao.
"Tunaiomba serikali fedha hizo zisitumike kupora demokrasia serikali ihakikishe Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), inafanya mchakato huru wa kuwapatia makamishna wapya ambao si makada wa CCM. Tunataka tume itakayosimamia uchaguzi kwa haki na haitapendelea chama chochote," anasema Dorothy.
Watanzania wamechoshwa na mchakato wa uchaguzi kwa makosa madogo yanayowafanya wagombea wa vyama pinzani waenguliwe na kwamba wanataka mawakala wa vyama vya upinzani wanaapishwa kwa wakati na wanapewe fursa sawa.
Akiwa mkoani Simiyu., Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa Chama cha ACT-Wazalendo Bara, Abduli Nondo, ananguruma, akisisitiza kuwa uchaguzi ndiyo fursa muhimu ya wananchi kuonyesha mamlaka yao kwa kuchagua viongozi wanao wataka.
Anakumbushia tangu nchi imepata uhuru imetawaliwa na chama kimoja cha TANU ambayo leo ni CCM na kwamba kuwapo kwao madarakani kwa muda mrefu wanawaona wananchi ni watumwa na wao ni mabosi.
"Tunakwenda kuchagua wabunge na madiwani kwa sababu tunataka uwakilishi wa mtu atakayetusemea kupata huduma za kijamii kama maji barabara na umeme.
"Mnapokwenda kuchagua mbunge mnachagua mwakilishi wa kwenda kuhakikisha anaisimamia serikali kwa manufaa ya wananchi. Leo hii bunge limejaa wanachama wa chama kimoja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED