YANAPOTAJWA majina; Job Ndugai na Stephen Wasira, yanatambulisha historia na kuibua hisia za siasa za Tanzania pamoja na harakati za uongozi ukiwamo pia wa ubunge.
Wasira akitinga kwa mara ya kwanza katika utendaji serikalini alikokwea hadi juu, tangu zaidi ya miaka 50 iliyopita, leo hii ni mzito ndiye, Makamu Mwenyekiti CCM Bara.
Huko ana jukumu la kuongoza sauti, matendo na propaganda za upande wao, anazoendelea kuzinadi kila kukicha katika mitaa mbalimbali ya nchi.
Ndugai, naye mnamo mwaka 2020, alichaguliwa kwa mara ya pili, kuwa Spika wa Bunge. Hapo akavuna asilimia 99.7 ya kura zote zilizopigwa bungeni kumpitisha.
Lakini, wastani wa mwaka mmoja na miezi kadhaa kazini, yakamkuta magumu kikazi akikabiliwa na shinikizo la wabunge wenzake walimtaka ajiuzulu, kikuu ni kauli ambayo haikukubalika kwa wenzake kuhusu utendaji serikalini.
Spika Ndugai alishutumiwa kukosoa baadhi ya miradi ya maendeleo serikalini, hata mwanzoni mwa Januari, 2022 akalazimika kujiuzulu wadhifa wake akiandika rekodi mpya ya kuachia ngazi nafasi hiyo.
Ni siku chache zimepita sasa, wawili hao Wasira na Ndugai wameibuka katika ubia wa kisiasa, ndani ya ziara ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, mkoani Dodoma, kunadi sera za chama na kuhakiki utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-25.
Katika staili ya pamoja, wote wakijumuika kuelezea mafanikio ya utendaji wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kisiasa na kiutawala, ila kila mmoja akawa na ya ziada kwa nafasi yake.
Wakati ziada kutoka kwa Wasira zikizama kujibu tuhuma dhidi ya chama chake, ya mbunge huyo wa Kongwa akajitoa kujiibua upya kisiasa, akitambulisha “alivyo Ndugai wa leo.”
WALICHONADI KWA UMMA
Wanasiasa mbalimbali wakitangaza dhamira zao kuwania ubunge wa majimbo, Ndugai naye hakuwa nyuma akiwa na hoja zake.
Akajinasibu kwa staili ya kujipigia debe la ubunge, akisema yeye pamoja na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwenye uchaguzi mkuu ujao wanayo miaka mingine mitano tena.
Huku akitumia msamiati “mbunge wetu Ndugai mitano tena, tumejipanga mtoa rushwa hawezi kutokea,” anajinasibu kwa historia aliyoitaja ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, wakifanya vizuri kulinganishwa na majimbo mengine ya mkoa wa Dodoma.
“Kongwa ni nguzo na tegemeo kubwa la mkoa wa Dodoma, sisi hapa tunashinda kwa ‘clean sheet’ (bila dosari), wajumbe wote wa serikali za vijiji na vitongoji vyote, wenyeviti, madiwani, mbunge ndiye usipime,” anatamba Ndugai.
WASIRA NA NONDO
Katika eneo la uchaguzi, kuna vyama vya upinzani ikiwamo, CHADEMA vimekuwa vikilalamika ‘kuibiwa kura’ katika uchaguzi mkuu uliopita, hata hivyo vikigawanyika katika azma ya ama kushiriki au kutoshiriki uchaguzi ujao mwaka huu.
Wakati ACT-Wazalendo ikitangaza kushiriki, CHADEMA imeweka msimamo wa kutoshiriki na kaulimbiu yake ‘No Reform No Election’ kwamba haitoshiriki uchaguzi hadi pale katiba ya nchi itakapofanyiwa marekebisho.
Katika staili inayoonekana Wasira anawajibu wapinzani, akatamka kwamba kama kuna wanasiasa wana hoja za kuwashawishi wapigakura, wazitoe na kama hawana wakubali kushindwa.
Naye akijinasibu kisiasa kukosoa ngome upinzani, akasema kuna sehemu ngome ya upinzani haisimamishi wagombea, kwa sababu hawana wawakilishi, akitumia mfano wa uchaguzi wa serikali za mtaa uliopita.
Hapo akatumia fursa ya mikutano yake kusisitiza hatua ya kuwapo amani na kipaumbele cha demokrasia kwa umma, akifafanua maana yake kwa kauli “si vurugu ila ni hoja, majadiliano na maelewano.”
Hapo Wasira, anatamka kuhusu itikadi inayowataka wananchi wasishiriki uchaguzi, akipinga kwa kauli ya swali:
“Huwezi kujisemea tu watu waandamane, hawawezi kuandamana wakashiba, unawatoa watu mashambani waandamane ili walale njaa halafu iweje? Hamna kitu…”
Anatetea chama chake CCM, kwamba kiko madarakani, Wasira akiwageukia wengine: “Sasa wengine wanatuuliza CCM mmekaa sana na sisi tunawauliza tulipotafuta uhuru tuliwaambia tunakaa mpaka lini? Tuna mkataba gani na ninyi…”
DEMOKRASIA
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara katika ziara hiyo anawakumbusha wanasiasa kuwa demokrasia si vurugu ila ni hoja, majadiliano na maelewano.
Anaeleza kama kuna wanasiasa wana hoja za kuwashawishi wapigakura wawakubali wazitoe na kama hawana wakubali kushindwa, akieleza kuwa kuna sehemu upinzani hawasimami kwa sababu hawana watu na kwamba uchaguzi wa serikali za mitaa anadai walishindwa hawakuwa na wagombea.
Kutokana na mivutano inayojitokeza kisiasa, kuelekea uchaguzi mkuu ujao, Wasira anasisitiza kwamba, maendeleo ya wananchi na taifa ni zao la amani, hivyo demokrasia ipewe kipaumbele, watu wajiepusha na uvunjifu wa amani.
Akizungumzia matokeo ya uchaguzi uliopita, anadai upinzani pamoja na kuweka wagombea wasio na sifa, jambo lililosababisha kushindwa, anakerwa na yanayoendelea sasa upinzani kuwataka wananchi wasishiriki uchaguzi, badala yake waandamane.
“Huwezi kujisemea tu watu waandamane, hawawezi kuandamana wakashiba, unawatoa watu mashambani waandamane ili walale njaa halafu iweje? Hamna kitu…”
HATUPUUZI HOJA
Wasira anaendelea kueleza kuwa hawapuuzi hoja za wengine, lakini mchakato wa uchaguzi utaendelea, huku akiwashukuru viongozi wa dini kwa kuwaongoza na kuwaunga mkono katika kuendelea na zoezi hilo kwa amani.
Anasema wanashukuru kuona nchi inaendelea kuwa na utulivu, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa mabadiliko makubwa katika eneo la utawala, akisisitiza kuwa mabadiliko aliyoyaita 'reform' ni suala endelevu na si la muda mchache.
Anaeleza hakuna sheria itakayotungwa watu wote wakaikubali, ndio maana kuna utaratibu wa kufanyiwa marekebisho, akisisitiza kwamba ‘hakuna reform’ inayokataliwa na si kwamba yaliyokwishafanyika yatadumu milele.
“Amani ni lazima tuilinde, kwa sababu ndani yake kuna haki, ukiiondoa wengi wataathirika wala si mtu mmoja ni wengi na ushahidi upo, tumepokea wakimbizi maelfu kutokana na kuvunjika kwa amani kwa majirani zetu,” anasema Wasira.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED