Wanawake wanapowania uongozi, cha kuangalia ni uwezo wao, si jinsi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:50 PM Jul 16 2025
Dk . Annanilea Nkya, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania na mwanamtandao wa haki na usawa kijinsia
Picha: Mtandao
Dk . Annanilea Nkya, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania na mwanamtandao wa haki na usawa kijinsia

JUMATANO iliyopita katika Kura Yangu Nguvu Yangu, tuliangalia umuhimu wa wanawake kuwa ndani ya mifumo ya uongozi. Tulipitia takwimu mbalimbali kuona kwa hapa Tanzania, ni kwa kiasi gani wanawake wameingia kwenye nafasi za maamuzi. Leo katika safu yetu, tutajikita katika kuangalia kwa nini idadi ya wanawake katika uongozi wa kisiasa ni ndogo licha ya jitihada kubwa zinazofanyika. Fuatana na Mwandishi Wetu, Dk. Joyce Bazira.

Kwa nini idadi ya wanawake wanaojitokeza kuwania uongozi wa kisiasa ni ndogo?  Kwa nini hata hao wachache wanaosimama kwa ujasiri kuomba ridhaa ya wananchi kuongoza, wengi hawapati ushirikiano au kuungwa mkono? Ziko sababu mbalimbali zinazoelezwa kwa chanzo cha hali hiyo.

Baadhi ya jamii hapa nchini wana mtazamo kwamba wanawake hawafai kuwa viongozi wa kisiasa. Kutokana na mila na desturi, baadhi ya jamii zinaamini kwamba kwamba viongozi wa kisiasa lazima wawe wanaume. 

Kwa mtazamo wao, wanawake wanapaswa kuangalia zaidi familia na kufanya majukumu ya nyumbani na si kazi za kisiasa, hivyo siyo sahihi kuwapa nafasi za uongozi zinazohitaji muda mwingi na kujitolea.

Kadhalika kuna mtazamo wa kihistoria kwamba wanawake ni dhaifu au hawana uwezo wa kufanya maamuzi makubwa, hivyo wanaona wanaume ndio wanafaa kuongoza.

Ubaguzi wa kijinsia ni tatizo jingine kubwa linalosababisha wanawake kutoungwa mkono pale wanapojitokeza kuwania nafasi za uongozi. Hata pale mwanamke anapokuwa na uwezo mkubwa wa kuongoza, bado anaachwa kutokana na jinsia yake. Matokeo ya hali hiyo, wanaume hushikilia nafasi nyingi za uongozi.

Kutotangazwa ama kuwekwa wazi kwa mchango mkubwa wa wanawake waliotangulia kuongoza, si sababu nyingine inayoifanya jamii isiamini uwezo wa wanawake kuongoza kwa mafanikio. 

Wapo wanawake wengi hapa nchini ambao wamefanya kazi kubwa kuunga mkono maendeleo ya kidemokrasia. Kadhalika wako wanawake viongozi ambao wamechangia katika kuanzisha na kutekeleza mikakati ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ikiwemo uanzishaji wa miradi ya mikopo kwa wanawake wachanga, uimarishaji wa sekta ya kilimo na biashara ndogo ndogo.

Wanawake viongozi wengi wamekuwa mstari wa mbele katika kupaza sauti kuhusu haki za wanawake na kupambana na ukatili wa kijinsia. Kadhalika ukifuatilia untendaji wa wanawake wengi viongozi, utabaini katika kipindi chao cha kuongoza yapo maeneo ambayo waliwekea mkazo tofauti na wanaume walipokuwa katika nafasi hizo.

Kwa mfano, sekta za elimu na afya, hasa kwa wanawake na Watoto, ni baadhi ya maeneo ambayo wanawake viongozi wametoa mchango mkubwa. Matokeo ya mchango huo ni ongezeko la idadi ya wasichana wanaosoma shule na kupunguza vifo vya mama na watoto. 

Licha ya wanawake kufanya kazi kubwa, wengi mchango wao haujatambuliwa wala kuandikwa kokote. Kutokana na hilo, jamii inaendelea kuwa gizani juu ya mabadiliko hayo makubwa yanayofanywa ama kuongozwa na wanawake wanaposhika uongozi wa kisiasa. 

Baadhi ya watu bado wana imani potofu kuhusu uwezo wa wanawake kufanya maamuzi. Wapo wanaoamini kuwa wanawake viongozi hufanya maamuzi kwa hisia na  si kwa uangalifu wa kitaalamu. Dhana hii potofu inaelezwa kuwa huchangia kwa kiasi kikubwa nani apewe nafasi kati ya mwanamke au mwanamume.

Mila potofu juu ya dhana ya uongozi ni sababu nyingine inayoelezwa kuchangia uwepo kwa idadi ndogo ya wanawake wanaochaguliwa kushika nafasi za uongozi wa kisiasa. Kihistoria, mara nyingi siasa zimekuwa na viongozi wa kiume pekee, hivyo jamii huona uongozi kwa wanawake kama jambo jipya na linalopingana na mfumo wa jadi.

Kutofahamu umuhimu wa usawa wa kijinsia na faida za wanawake katika uongozi, ni sababu nyingine inayochangia uwepo wa idadi ndogo ya wanawake katika uongozi wa kisiasa. 

Hizi ni baadhi ya sababu za msingi za dhana hizi, lakini ni muhimu kuelewa kwamba ni mitazamo inayopaswa kubadilika kwa manufaa ya jamii na maendeleo ya kila mtu.

Zipo faida nyingi zinazopatikana pale wanawake wanaposhikilia nafasi za uongozi wa kisiasa. Kwa mfano, ushiriki wa wanawake katika uongozi unasaidia kuwepo kwa maamuzi yanayozingatia usawa na haki kwa makundi yote.

Wanawake na wanaume wanatazama mambo ya mitazamo tofauti. Kwa hiyo timu ya uongozi inapokuwa na jinsia zote mbili, maana yake ni kwamba kutakuwa na mitazamo tofauti katika kuibua mambo, kujadili na hata kufanya maamuzi. Hali hii inaweza kuleta mabadiliko chanya katika sera, hasa kuhusiana na masuala ya familia, elimu, afya, na haki za wanawake na watoto.

Kadhalika wanawake kuwa katika uongozi ni muhimu kwa kukuza demokrasia kamili ambapo kila mtu, bila kujali jinsia, ana nafasi ya kushiriki katika mchakato wa maamuzi.

Wanawake wengi wakiwa viongozi, wanahamasisha sera zinazolenga ustawi wa familia na jamii, kwa mfano kupunguza ukatili wa kijinsia, kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto, na kuhakikisha usalama wa watoto.

Viongozi wanawake hutoa mfano kwa wasichana na wanawake wengine kujiamini na kujiunga na siasa au nyanja nyingine za uongozi na ushawishi.

Kuwepo kwa wanawake katika uongozi kunasaidia kupambana na unyanyasaji wa kijinsia na ubaguzi katika maeneo ya kazi na jamii kwa ujumla.

Hizi ni baadhi ya sababu za msingi za dhana zinazochangia uwepo kwa idadi ndogo ya wanawake wanaojitokeza kuwania nafasi za uongozi wa kisiasa na hatimaye kuathiri idadi ya wale wanaoingia kwenye nafasi za maamuzi. Ni vyema tukaelewa kwamba mitazamo potofu inapaswa kubadilika kwa manufaa ya jamii na maendeleo ya kila mtu.

Swali la kufikirisha:

Ni mababiliko yapi yamefanywa na kiongozi mwanamke katika eneo lako ? 

Tuma majibu yako kupitia : joyce_bazira