AKILI mnemba (AM) ni teknolojia mpya inayoendesha maisha duniani hasa kwa nchi zilizoendelea.
AM au kwa Kiingereza Artificial Intelligency -AI hutatua changamoto mbalimbali zinazomkabili binadamu kwa ufanisi na weledi hata kwa gharama nafuu.
Profesa Edward Hosea, anazungumzia AM kwenye mafundisho ya Injili ya Mtandaoni yanayotolewa na Kanisa la Kisabato wiki iliyopita, anachambua AM kuwa ni zao la akili ya binadamu na hakuna shida inayohitajika kwa maendeleo ya dunia na Tanzania pia.
Akisema ni akili ya binadamu anayeunda mashine au kompyuta zenye uwezo wa kasi kubwa ya ufahamu na utambuzi mithili ya akili za watu.
Inafafanua kuwa zinaendeshwa kwa program za ‘aligorithm’ ambazo lengo lake ni kuandaa na kufuata taratibu na kanuni za mahesabu au shughuli nyingine na kwa kutumia kompyuta kutatua tatizo na kupata ufumbuzi na kupunguza changamoto zinawakabili watu na dunia.
Anasema AM au AI ni nadharia zilizoelezwa kwa mara ya kwanza na John McCarthy, mwanasayansi wa kompyuta wa Marekani miaka ya 1950.
Anawaambia watu mbalimbali wanaofuatilia mafundisho hayo kwa mitandao kuwa ubunifu na teknolojia ni mambo yanayotoka kwa Mungu, aliyempa mwanadamu ujuzi na maarifa ili atawale dunia akitumia akili na maarifa.
Hosea ambaye ni mwanasheria mbobezi, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), anasema Mungu amempa binadamu akili na vitu vingi ili avitawale mfano, madini, bahari na rasilimali nyingi ajiletee maendeleo na mafanikio ili kumjua Mungu ndiyo maana sayansi na teknolojia zinahitajika.
Profesea Hosea anasema AI ikitumika ipasavyo kwa malengo ya kiufanisi haina tatizo, lakini inapotumiwa kuhadaa na kudhalilisha haipendezi.
Anatoa mfano kuwa inaweza kutumika kuonyesha mkuu wa nchi anazungumza jambo ukadhani ni kweli wakati ni uongo, kadhalika ikamwonyesha anacheza midundo ukafikiri ni ukweli lakini ni udanganyifu.
“Teknolojia hii inahitajika ili itumike kusaidia mazingira magumu yanayomkabili binadamu. AI isionekana kuwa ni kitu kibaya ni zana ya uchambuzi -analysis, ujuzi na maarifa kwa ajili ya maendeleo.” Anaongeza Profesa Hosea.
Anasisitiza kuwa ni maarifa kutoka kwa Mungu, AM isichukuliwe kuwe ni kitu kibaya na kwamba dunia ya sasa inatumia karibu asilimia 90 ya akili mnemba kuendesha maisha harakati zake kwa kasi.
AM ambayo ni mifumo ya kompyuta inayofanyakazi ambazo zinahitaji akili ya binadamu, kama kuona, kutambua sauti, kufanya maamuzi au kutafsiri lugha, inatumika karibu kila mahali leo.
Ndizo roboti, ndege zisizo na rubani au droni, magari yanayojiendesha bila dereva, kamera za CCTV, malipo ya kielektroniki mfano ya kutumia ‘kontroli namba’ madaktari wa kiroboti.
Akili mnemba ni kompyuta, injini za kutafuta taarifa mfano tovuti ya Google, YouTube, Tiktok na Netflix, Google Assistant, Siri na kwenye roboti za mazungumzo zipo ChatGPT na Gemini.
HATARI ILIPO
Licha ya AI kuwa zana (tool) kwa binadamu kufanya kazi kwa ufanisi, kasi na kupata maendeleo ina hatari inapotumika vibaya inaeneza uongo, chuki, uzushi unaosambaa kwa kasi kwenye mitandao.
AI kwenye TEHAMA kinachotia hofu ni ujumbe au maudhui yanayosambazwa yakihusisha picha, video, maneno, maandishi, sauti, zinazounganishwa na matendo wakati mwingine ya kiudhalilishaji.
Mfano, hivi karibuni baada ya Papa Leo XIV kuchukua uongozi wa Kanisa Katoliki, amekuwa mlengwa wa kazi za akili mnemba, akidaiwa kuzungumza habari zilizoenea karibu dunia nzima, kumsifu Rais wa Burkina Faso na kumponda Donald Trump wa Marekani.
Papa anaonekana kwenye video akijibu barua ya Rais Ibrahim Traore wa Burkina Faso, katika mkanda unaopatikana kwenye YouTube.
Anasema: "Nimesoma maneno yako sio mara moja, lakini mara nyingi. Kwa sababu kwa sauti yako sijasikia tu hasira ya rais, lakini kilio cha haki cha bara lililojeruhiwa kwa muda mrefu na sababu mbili za kupuuzwa na unyonyaji."
Papa ananukuliwa kwenye video ambayo imesambazwa kwenye majukwaa mengi ya kijamii kama X au twiter, Youtube na Tiktok.
Video hiyo ya dakika 36 ilichukua picha ya mkutano wa Papa na waandishi wa habari Mei 12 mwaka huu na kuunda picha na sauti ikiitumia mbinu ya kurekebisha midomo ya Papa ili kuendana na rekodi ya sauti inayozalishwa na ujumbe huo wa AM, inathibitisha Vatican News, tovuti rasmi ya habari ya Papa.
Papa ni mmoja tu wa watu mashuhuri wanaotumiwa na wafuasi wa Traore ili kukuza sura yake - nyimbo na video zinazozalishwa na AM ili kumsifu kiongozi huyo kijana wa Afrika.
Wengine walioathiriwa ni watu maarufu kama Rihanna na Beyonce wanamuziki maarufu wanawake wa Marekani na Justin Bieber mwimbaji na mwandishi maarufu wa nyimbo wa Canada.
PAPA Vs TRUMP
Kwa kutumia AM au akili mnemba, Papa anadaiwa kumkosoa vikali Rais wa Marekani Donald Trump katika video iliyosambazwa kwenye TikTok na Instagram.
Anasema: "Trump, sera zako za uhamiaji ambazo umetekeleza ni kupinga na kukanyaga waziwazi mafundisho ya kanisa na ahadi za ndoto ya Marekani."
Papa Leo XIV inadaiwa kupinga vikali kila kitu ambacho Trump anasimamia huko Marekani, ni katika video zinazobadilishwa.
Vatican inasema Papa hajawahi kutoa taarifa kama hizo na kwamba hotuba, zake, maandishi ya Papa yote yapo katika tovuti rasmi ya Vatican na habari za shughuli zake zinapatikana kwenye Vaticannews kila siku.
Kuna maelezo kuwa video hizo si za kweli bali ni hila kumtumia Papa Leo kutetea kila ambacho wanaoandaa maudhui wanakilenga walichokusudia.
MASHOGA WAIBUKA
Papa Leo XIV anadaiwa alipuuza kwa makusudi bendera ya upinde wa mvua ya wanaojiita wasagaji, mashoga, watu wa jinsi mbili, waliobadili jinsi, watu wa jinsi tofauti na wasio na uhakika wa jinsi zao(LGBTQ) kwa kuangalia upande mwingine alipoikaribia bendera hiyo," ni ujumbe uliowekwa mtandaoni X uliodai ulitazamwa na zaidi ya watu milioni 12.
Uhakiki unabaini kuwa si kweli, ikikanusha Vatican News na kuongeza kuwa bendera ya rangi nyingi ya "upinde wa mvua" katika video si ya LGBTQ ni bendera ya Amani ya Italia yenye neno la Kiitaliano la amani juu yake.
Kwa ujumla AM ni zao la kiteknolojia ambalo lina faida lakini kama litatumika vibaya kuchora vibonzo, kutengeneza video bandia, picha na sauti za kudhalilisha wengine itaongeza changamoto kwa wale wasioweza kutafautisha uzushi na ukweli.
Teknolojia hiyo inaweza kuleta chuki, uhasama na hata vita pale itakapowafikia wenye hasira kali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED