Iringa kuwa na ‘Machinga Complex’ yao

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 01:46 PM Sep 07 2025
Mgombea urais CCM, Samia Suluhu Hassan
Picha: Romana Mallya
Mgombea urais CCM, Samia Suluhu Hassan

MKOA wa Iringa umeahidiwa kujengewa Machinga Complex, ikiwa ni ahadi ya mgombea urais CCM, Samia Suluhu Hassan, aliyotoa leo, Septemba 7, 2025, mkoani humo.

Akizungumza na maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa kampeni mkoani humo, Samia ameahidi akieleza ataimaliza kabla ya muda wake wa kazi kuisha, ili machinga na mama lishe wafanye biashara zao vizuri.

Dk. Samia amesema manispaa imejenga ofisi ya machinga mkoa na yeye aliahidi kutoa fedha kujenga ofisi hizo nchi nzima, ambapo alitoa fungu la fedha TAMISEMI wakajazia zikapelekwa halmashauri wakasimamia ujenzi huo.

“Niwahakikishie kuendelea kuboresha mazingira yenu ya biashara. Tumeboresha huduma za kijamii maeneo ya elimu, afya, maji miaka mitano iliyopita,” amesema.

Samia alisema katika kukuza uchumi na ajira kwa vijana, Iringa imeongeza viwanda, ambapo wakati akiiingia madarakani ulikuwa na viwanda 24 vikubwa na sasa viko 40, na kuahidi kuongeza na kuboresha kongani za viwanda.