‘Hatuwezi kudharau mwiba, kisa misumari imelala’

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 02:19 PM Sep 07 2025
Mgombea urais CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, akihutubia mkutano wa kampeni Chamwino
Pichja: Romana Mallya
Mgombea urais CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, akihutubia mkutano wa kampeni Chamwino

MGOMBEA urais CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema hata kama upinzani haupo katika uchaguzi mkuu mwaka huu, hawawezi kudharau mwiba kisa misumari imelala.

Akizungumza  leo, Septemba 7, 2025 na wananchi wa Mlowa, Jimbo la Chamwino, akiwa njiani kuelekea Dodoma,  Samia amesema: 

“Mbunge wenu amesema hapa, wanajiamini huko kwa nini CCM, mama anatumia nguvu sana, wakati upinzani haupo.

“Waswahili wanasema anayedharau mwiba ukimchoma mguu unaota tende, sasa usisubiri mpaka uchomwe na msumari, hata mwiba  lazima uushughulikie.”

Amesema kama misumari imelala, miiba iliyochomoza lazima waishughulikie ipasavyo.

“La pili wana CCM wameridhishwa na kazi nzuri iliyofanyika ndio maana kila tunapokanyaga kuna utitiri wa watu wengi kwa sababu wameridhishwa na kazi iliyofanywa na serikali, kwao ndio jambo kubwa kuliko lolote. 

“Sina wasiwasi na mkoa wa Dodoma, lakini uungwana unapokuwa na haja unapaswa kwenda kwa mwenzio kwa heshima,” amesema na kuomba kura kwa mafiga matatu kupitia CCM, ambayo ni nafasi ya Rais, Wabunge na Madiwani.