18 CHADEMA wakamatwa, mkusanyiko usio halali

By Mary Mosha , Nipashe
Published at 11:38 AM Sep 07 2025
SACP Saimon Maigwa
PICHA: MTANDAO
SACP Saimon Maigwa

JESHI la Polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia Watuhumiwa 18 akiwemo Katibu Mwenezi Baraza la Vijana Taifa wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema), Felius Kinimi kwa tuhuma za kufanya mikusanyiko iliyo kinyume na Sheria sambamba na kupanga njama za kuhamasisha vurugu na kuhatarisha amani na usalama nchini.

Akithibitisha kukamatwa kwa watu hao, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, SACP Saimon Maigwa amesema kuwa, watu hao wamekamatwa katika eneo la Sambarai Kibosho wilayani Moshi. 

Alisema kuwa, Jeshi hilo limekuwa likiwafuatilia sambamba na kukusanya ushahidi na jana walipokuwa wanakwenda kutekeleza vitendo ambavyo ni kinyume cha Sheria ndiyo likafanikiwa kuwatia nguvuni.

Alisema kuwa, ushahidi unakamilishwa ikiwa ni sambamba na kuwahoji ili hatua zingine za kisheria zifuate na kutumia nafasi hiyo kuonya yeyote anayepanga njama za kuhamasisha na kufanya vurugu ili kuhatarisha amani, utulivu na usalama hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi na baada ya uchaguzi halitasita kuwakamata ili Sheria iweze kuchukua mkondo wake.

"Niwaonye yeyote anayepanga njama za kuhamasisha na kufanya vurugu ili kuhatarisha amani utulivu na usalama Jeshi la polisi hatutasita kuwachukulia hatua za haraka kabla ya jambo hilo kutimia ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa" amesema SACP Maigwa.