Mgombea mwenza wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Emmanuel Nchimbi, amesema endapo wananchi watampatia ushindi mgombea urais wa chama hicho, Dk. Samia Suluhu Hassan, serikali yake katika siku 100 za mwanzo itatoa ajira mpya 5,000 kwa kada ya afya na 7,000 kwa sekta ya elimu ili kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii nchini.
Dk. Nchimbi ameyasema hayo leo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Kashai, Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, ikiwa ni siku yake ya pili ya kampeni mkoani humo kwa lengo la kumnadi mgombea urais pamoja na wagombea wa ubunge na udiwani wa CCM.
Amesema ajira hizo mpya zitatokana na uboreshaji wa miundombinu ya afya na elimu utakaofanyika mara baada ya CCM kuunda serikali.
Aidha, Dk. Nchimbi amesema Dk. Samia ameazimia kuanza kwa kushughulikia changamoto ya bima ya afya, hasa kwa makundi maalumu ikiwemo wajawazito na wazee, kwani makundi hayo yamekuwa yakikumbana na vikwazo pindi yanapohitaji huduma hospitalini.
Ameongeza kuwa serikali pia itahakikisha huduma za matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza zinatolewa bure, kutokana na changamoto kubwa ya maradhi hayo kwa wananchi wengi.
Kuhusu mipango ya maendeleo katika Manispaa ya Bukoba, Dk. Nchimbi amebainisha kuwa serikali itajenga vituo vitatu vya afya vya kisasa, zahanati nne, shule mpya za msingi, vyumba vya madarasa 136 pamoja na mradi wa kusambaza huduma za umeme.
Kwa upande wa miundombinu ya usafiri, amesema serikali imepanga kujenga jengo jipya la abiria na vibanda vipya katika eneo la stendi, ambapo maandalizi ya awali tayari yameanza.
Aidha, amesema serikali ya CCM itatenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kukopesha vikundi vya vijana nchini, ili kuwawezesha kujiendeleza kiuchumi.
Akizungumzia sekta ya kilimo, Dk. Nchimbi amesema baada ya uchaguzi serikali itajenga kiwanda cha kutengeneza mvinyo wa ndizi ili kuwanusuru wakulima dhidi ya hasara inayojitokeza kutokana na kuharibika kwa ndizi mbivu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED