Wananchi zaidi ya 60,000 Mtakuja kupata huduma za afya karibu

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:58 PM Sep 06 2025
Wananchi zaidi ya 60,000 Mtakuja  kupata huduma za afya karibu
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Wananchi zaidi ya 60,000 Mtakuja kupata huduma za afya karibu

Changamoto ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma ya afya hasa upasuaji pindi mjamzito anaposhindwa kujifungua kwa njia ya kawaida kwa wakazi wa kata ya Mtakuja Manispaa ya Geita iko mbioni kumalizika baaada ya serikali kutumia zaidi ya Sh 500 milioni kujenga kituo cha afya katika kata hiyo.

Kituo hicho mbali na kuwasaidia wajawazito pia kitahudumia wananchi zaidi ya 61,000 kutoka katika mitaa mitano ya kata hiyo. Akizungumza wakati wa mbio za mwenge wa Uhuru uliotembelea eneo hilo kwa ajili ya uwekaji wa jiwe la msingi , Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Yefred Myenzi  amesema fedha hizo zimetumika kujenga chumba cha upasuaji,jengo la maabara na wodi ya wazazi.

“Wananchi wa mitaa mitano ya Mtakuja  hawakuwa na kituo cha afya wanazahanati moja ya Mpomvu hii iliwalazimu kusaafiri hali hospitali ya Mji kupata huduma lakini kituo hiki kikikamilika na kuanza kutoa huduma wananchi waliokuwa wakilazimika kwenda mbali sasa watapata huduma za upasuaji,vipimo mbalimbali hapahapa kwenye maeneo yao,”

Mbali na ujenzi wa kituo cha afya Mwenge wa Uhuru umetembelea na kukagua miradi 11 ya maendeleo yenye thamani ya Sh bilioni 145.8  ukiwemo mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari  Mbabani iliyopo kata hiyo, ambao umewaondolea wanafunzi adha ya kutembea zaidi ya km 10  kila siku kufuata shule.

Awali wanafunzi wa mtaa wa Mbabani walilazimika kwenda shule za Shantamain na Mtakuja ,hali iliyosababisha baadhi yao kuacha shule na wengine kuwa watoro ,jambo lililoathiri ufaulu wao.

Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye kituo cha afya Mtakuja,kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Ismail Alli Ussi, amesema serikali inaendelea kufanya kufanya jitihada za kuhakikisha huduma za afya na elimu zinawafikia wananchi kote nchini.

“Serikali imejenga hospitali na vituo vya afya kote nchini.Wakurugenzi endeleeni kutengfa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu niwaombe na wannachi mshirikiane na watoa huduma ili huduma bora ziendelee kutolewa ,”amesema Ussi

Baadhi ya wakazi wa kata ya Mtakuja wamesema kupatikana kwa kituo cha afya na shule kwenye kata hiyo umekuwa mkombozi mkubwa kwao. Hamis Sagaika amesema awali wajawazito walilazimika kupanda bodaboda kwenda mjini kuwahi hospitali kutokana na kukosa kituo cha afya, lakini sasa hofu ya kujifungulia njiani au kupoteza mtoto imepungua.