Samia: Tunajipanga kufikia megawati za umeme 8,000

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 01:35 PM Sep 07 2025
Mgombea wa urais CCM, Samia Suluhu Hassan
Picha: Romana Mallya
Mgombea wa urais CCM, Samia Suluhu Hassan

MGOMBEA wa urais CCM, Samia Suluhu Hassan, ameweka wazi Tanzania anayoidhamiria, yenye kutoa matumaini kwa wananchi kwa kujikwamua kiuchumi, kutokana na maboresho aliyolenga kuyafanya sekta tofauti za uchumi.

Amesema katika nishati wametoka megawati 1,600 mwaka 2020 na mpaka mwaka huu 2025, zimefikia megawati 4,000 na sasa wamejipanga kufikisha megawati 8,000 wakitumia vyanzo mbalimbali vikiwamo maji, upepo na joto ardhi.

Samia ametoa kauli hiyo leo, Septemba 7, 2025, Iringa mjini katika mkutano wa kampeni za chama hicho uliofanyika uwanja wa Samora, akiendelea kunadi sera na Ilani ya CCM,  ili kuomba ridhaa kwa wananchi kumchagua.

Amesema kwa ukanda huo, wategemee kupata umeme mwingi wa joto ardhi na upepo.

“Tunajipanga vyema, ili umeme uwe ndio msingi na kichocheo cha maendeleo ya nchi yetu,” aliahidi.

Wakazi wa Iringa
Dk. Samia amesema kwa upande wa nishati, aliahidi kufikisha miundombinu ya umeme katika vijijini 360 vilivyoko Iringa na kwingineko na wamefanya hivyo na sasa kazi inaendelea katika vitongoji, vingi vimeshapata.

Amesema kwa Iringa mjini wamefikisha huduma hizo katika mitaa 189 kati 192, iliyobaki wakandarasi wanaendelea.

“Pamoja na kusambaza umeme Tanzania nzima, bado tuna kazi ya kuongeza  uzalishaji umeme, ili uweze kutosha.”