Mila, imani potofu visitafune maisha ya mama na mtoto

Nipashe
Published at 01:03 PM Oct 08 2025
Malezi bora ni ustawi mzuri wa jamii
Picha: UN
Malezi bora ni ustawi mzuri wa jamii

KATIKA karne ya 21, ambapo dunia inazungumza kuhusu teknolojia ya kisasa, upasuaji wa kutumia roboti na tiba za kisasa za magonjwa sugu, bado tunashuhudia mama mjamzito akipoteza maisha kutokana na dawa za kienyeji za kufungua njia au kwa kuchelewa kufika hospitalini kutokana na imani za kishirikina.

Hili ni jambo la kusikitisha na linaibua maswali mazito juu ya mafanikio ya juhudi za afya ya uzazi katika maeneo ya vijijini, hasa wilayani Magu, mkoani Mwanza.

Ripoti kutoka wilayani Magu tuliyochapisha jana na leo, inaonesha taswira ya kushangaza na ya kuhuzunisha. Inaweka wazi kuwa licha ya kuwapo hospitali, zahanati na vituo vya afya, bado wanawake wajawazito wanacheleweshwa kupata huduma bora kwa sababu ya kuamini nguvu za waganga wa jadi, mila potofu na kutoelewa hatari ya kuchelewa kupata huduma za uzazi.

Matokeo yake ni vifo vya kinamama na watoto ambavyo vingeweza kuzuilika kwa elimu na huduma sahihi.

Ni dhahiri kuwa suala hili si la afya pekee. Ni la kijamii, kiutamaduni na kiuchumi. Mifano ya kinamama kama Suzana Kayenji na Rozimary Faustine, wanaoelezea kusuasua kwa huduma kutokana na imani za jadi, inaonesha jinsi maisha ya wanawake wengi yanavyohusishwa zaidi na imani badala ya sayansi. 

Rozimary, ambaye alinusurika kufariki dunia, baada ya kukumbatia tiba ya kisasa, anathibitisha kuwa mabadiliko ya mtazamo yanaweza kuokoa maisha.

Katika jamii ya Magu na maeneo mengi ya vijijini nchini, bado kuna imani potofu kuwa kuzaa watoto wengi ni heshima, na kuwa uzazi wa mpango ni hila za kisasa za ‘kuharibu kizazi’.

Wapo wanaume wanaodhani wake zao watakuwa “waasi wa ndoa” au watapoteza uaminifu endapo watatumia njia za uzazi wa mpango. Hili ni tatizo la kijinsia ambalo linahitaji kukabiliwa kwa ukali na maarifa.

Ni jambo la kusikitisha zaidi kuona kuwa vifo vya wajawazito na watoto wachanga wilayani Magu vilifikia 279 ndani ya kipindi cha miaka minne, sababu kuu zikiwa ni mila, ukosefu wa elimu na kuamini waganga wa jadi kuliko madaktari.

Takwimu hizi hazipaswi kuendelea kutazamwa kama habari za kawaida. Zinapaswa kuchukuliwa kama tishio kwa usalama wa kizazi kijacho.

Serikali ya Wilaya ya Magu, kupitia viongozi wake kama Mkurugenzi wa Halmashauri na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, imeonesha nia njema ya kushughulikia changamoto hii kwa kutoa elimu, kushirikiana na waganga wa jadi, na kuhimiza matumizi ya huduma za kisasa.

Hili ni jambo la kupongezwa, lakini halitoshi ikiwa jamii husika haitabadilisha mitazamo na imani inazozikumbatia kwa nguvu zote.

Viongozi wa jamii, wazee wa kimila, viongozi wa dini, na hususan wanaume, wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kuwaelimisha wanawake, vijana na watoto kuhusu umuhimu wa kliniki za wajawazito, uzazi wa mpango na kuachana na mila hatarishi.

Hili si jukumu la serikali pekee. Ni wajibu wa kila raia mwenye dhamira ya kweli ya kuona Tanzania inazalisha kizazi chenye afya bora.

Waganga wa jadi kama Bibi Nyamongo, waliokiri bayana kuwa huduma za hospitalini ni bora na salama zaidi, wanapaswa kuwa sehemu ya suluhisho, si tatizo.

Wao wawezeshwe kuwa mabalozi wa afya vijijini kwa kuwahimiza wateja wao kufika hospitalini mapema. Utaifa wetu hauwezi kujengwa kwa misingi ya ujinga, woga na usiri wa Kiafrika usio na mantiki ya kiafya.

Iwapo taifa likiamua kwa dhati kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi kwa njia ya kukabiliana na mila potofu, kutoa elimu ya afya vijijini, kuongeza huduma rafiki kwa wajawazito na kuvunja miiko inayozuia wanawake kupata huduma bora, basi tunaweza kuona mabadiliko makubwa ndani ya muda mfupi.

Tukumbuke: Mtoto na mama wanapokuwa salama, jamii nzima imeokolewa. Tusikubali mila na imani potofu viendelee kutafuna maisha ya mama na mtoto.