KILA mwaka ifikapo Oktoba 5, dunia huadhimisha Siku ya Walimu Duniani kama njia ya kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa walimu katika jamii.
Hata hivyo, maadhimisho haya kwa upande wa Tanzania yanaendelea kufanyika katika kivuli cha ukimya na huzuni kwa maelfu ya walimu wa kujitolea wanaojitwika jukumu la kufundisha bila ajira, bila malipo ya maana, na mara nyingi bila hata kutambuliwa rasmi na mfumo wa elimu.
Hili ni kundi ambalo licha ya kuonekana kama sehemu ya suluhisho la upungufu wa walimu shuleni, linapuuzwa na kutumika kama nguvu kazi ya muda bila kuwa na mpango madhubuti wa kulithamini, kulijengea uwezo, wala kulipa matumaini ya baadaye.
Walimu wa kujitolea wamegeuzwa kuwa “mashujaa wa dharura” ambao hufanikisha malengo ya elimu kitaifa, lakini baadaye husahaulika mara tu ajira mpya zinapotangazwa.
Mifano hai ya hali hii imetolewa na walimu kama Mwalimu Elisha Mfyumbula kutoka Mbeya, ambaye kwa miaka mitano amekuwa akifundisha bila ajira wala mshahara wa kueleweka.
Akiwa amejaa uchungu, anasimulia jinsi walimu wa kujitolea wanavyonyimwa hata heshima ya msingi na kushindwa kumudu hata nauli ya kufika kazini.
Kwa kiwango cha chini kabisa, anapendekeza kuwapo posho rasmi, hata kama ni nusu ya mshahara wa walimu waajiriwa, ili angalau walimu hawa wapate matumaini ya kuendelea kuhudumu.
Ni jambo la kusikitisha kwamba walimu hawa, licha ya kuonesha uzalendo wa hali ya juu, bado hukumbwa na dharau na kejeli kutoka kwa baadhi ya walimu waliopo kazini.
Wanaelezwa kama watu wa daraja la pili katika taasisi zao, na hali hii imekuwa chanzo cha kuvunjika moyo kwa wengi.
Matukio ya kubezwa mbele ya wanafunzi, kutopewa nafasi kwenye uamuzi wa kitaaluma na kukosa vifaa vya kufundishia ni miongoni mwa madhila yanayowakumba kila siku.
Kwa upande mwingine, ipo mifano ya walimu wa kujitolea waliotoa matokeo ya kipekee, kama Bernald Mwakajila aliyefundisha somo la hisabati hadi wanafunzi wake 100 kufaulu kwa alama "A".
Huu ni uthibitisho kwamba walimu wa kujitolea siyo watu wa kupuuzwa, bali ni rasilimali muhimu ambayo haijatunzwa ipasavyo. Badala ya serikali kuacha vipaji hivi vipotee, inapaswa kuwa na mfumo wa wazi wa kutambua, kuendeleza na kuwajengea walimu hawa msingi wa ajira ya kudumu.
Aidha, baadhi ya walimu kama Mwajuma Munga kutoka Rufiji, wamefundisha kwa miaka minne wakisubiri ajira isiyokuja. Wengine wanaishi katika mazingira duni, huku nyumba za walimu shuleni zikiwa wazi.
Ni jambo linalotia huzuni kwamba mwalimu wa kujitolea hulazimika kulala katika chumba chenye dari linalovuja, ilhali nyumba ya walimu haina mkazi. Huu ni uzembe wa kiutawala usiokubalika.
Pia, changamoto ya teknolojia imeendelea kuwa kikwazo kwa walimu wengi walioko shuleni, hasa wale wa kujitolea ambao hawana fursa ya mafunzo ya mara kwa mara.
Serikali inapaswa kuhakikisha walimu wote, wakiwamo wa kujitolea, wanapatiwa mafunzo ya teknolojia ili waendane na mabadiliko ya kisasa katika sekta ya elimu.
Katika muktadha huu, kauli ya Katibu wa Umoja wa Walimu Wasio na Ajira (NETO), Daniel Edgar, ina uzito wa kipekee. Alieleza bayana kuwa mfumo wa sasa unawaumiza walimu wa kujitolea na kupotosha taswira halisi ya uhaba wa walimu nchini.
Huu ni ukweli mchungu ambao serikali haiwezi tena kuufumbia macho. Ni wakati wa kuweka sera madhubuti ya kuwatambua walimu wa kujitolea, kuwathamini kwa posho halali, na hatimaye kuwaajiri kwa mujibu wa sifa na uwezo waliouonesha kwa vitendo.
Tanzania haiwezi kuwa na mfumo thabiti wa elimu kama haitawajali walimu wake wote, bila kujali kama wana mikataba au la. Walimu wa kujitolea siyo watu wa muda; ni watu waliochagua taaluma ya ualimu kwa moyo.
Kuwathamini ni kuwekeza katika elimu bora, na hatimaye, taifa lenye maarifa. Serikali inapaswa kuchukua hatua sasa – si kwa huruma, bali kwa haki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED