Mwakinyo: Nipo tayari kupigana yeyote maslahi yakiwa mazuri

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 02:59 PM Aug 15 2025

Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo.
Picha:Mtandao
Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo.

Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo, amesema yupo tayari kupambana na bondia yeyote, mradi maslahi ya pambano yatakuwa mazuri.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari kuelekea pambano lake lijulikanalo kama Dar on Boxing Day litakalofanyika Desemba 26 mwaka huu mkoani Mwanza, Mwakinyo alisema anaamini uwezo wake kwenye mchezo wa ngumi unaweza kumkutanisha na mpinzani wa aina yoyote.

“Nipo tayari kupigana na bondia yoyote, ilimradi nipate maslahi ninayoyahitaji, kwani najua nina uwezo mkubwa kwenye ngumi,” amesema Mwakinyo.

Ameongeza kuwa anaendelea na mazoezi kwa ajili ya kuhakikisha anafanya vizuri katika pambano hilo, huku akibainisha kuwa mpinzani wake atatangazwa baadaye.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kampuni ya Peak Time Sport Agency, Bakari Khatibu, alisema lengo la pambano hilo ni kuinua vipaji vya mabondia waliopo katika ukanda wa Ziwa na kuendeleza sifa ya mchezo wa ngumi nchini.

“Lengo la kufanya pambano hilo ni kuinua vipaji vya mabondia waliopo kanda ya Ziwa pamoja na kuendelea kuutangaza mchezo wa ngumi,” amesema Khatibu.

Amesema mpinzani wa Mwakinyo atatangazwa hivi karibuni ili mashabiki na wadau wa ngumi waweze kumfahamu mapema.