KWA mara ya kwanza katika mashindano ya CHAN yanayofanyika kwa ushirikiano wa nchini tatu za Afrika Mashariki, Tanzania, Kenya na Uganda, yameweka historia kwa timu zake zote kufuzu hatua ya robo fainali.
Timu zote hizo zimekuwa vinara wa makundi yao na kujihakikishia nafasi ya kucheza robo fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo.
Hapo awali, Uganda haikuwahi kupita hatua ya makundi, Tanzania ilikuwa imetolewa mara mbili, na Kenya hii ndio mara ya kwanza inashiriki michuano hiyo.
Katika Kundi A, Kenya imeongoza kundi lake hilo lililokuwa linaitwa ‘Kundi la Kifo’ likijimuisha timu za Morocco, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Zambia na Angola, ikijikusanyia pointi 10.
Kenya sasa itacheza na Madagascar kwenye robo fainali, Ijumaa.
Tanzania ambayo ilikuwa Kundi B imeongoza kundi hilo ikiwa na pointi 10, lililokuwa na timu za Madagascar, Burkina Faso, Mauritania na Jamhuri ya Kati.
Tanzania sasa itacheza na Morocco kwenye hatua ya robo fainali, Ijumaa.
Uganda nao wameongoza kundi C wakiwa na pointi saba, ambapo walikuwa na timu za Afrika Kusini, Algeria, Niger na Guinea.
Uganda sasa inakutana na timu iliyoshika nafasi ya pili jana usiku kutoka Kundi B, linaloundwa na Sudan, Senegal, Congo na Nigeria. Hii ni baada ya kutoka sare ya mabao 3-3 juzi dhidi ya Afrika Kusini, kwenye mechi yao ya kuhitimisha hatua ya makundi.
Kocha wa Uganda, Morley Byekwaso, baada ya mchezo huo, alisema: "Kwa hakika tumeweka historia yetu, tumefuzu hatua ya robo fainali ya CHAN kwa mara ya kwanza, hivyo lazima tujipongeza kwa kile tulichofanikiwa kukifikia. Tumeleta furaha kubwa kwa mashabiki wetu na wachezaji wamecheza kwa moyo wote.
“Tunaiangalia robo fainali kwa umakini mkubwa sana, timu zote zilizofuzu kwa hatua hii zina kiwango cha juu, hivyo lazima tukapambane sana.”
Hatua ya robo fainali ya michuano hiypo itaanza kutimua vumbi Ijumaa wiki hii katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ambapo Tanzania 'Taifa Stars' itavaana na Morocco, mechi ikipigwa saa 2:00 usiku.
Ijumaa hiyo pia mchezo wa mapema wa robo fainali utakuwa wa saa 11:00 jioni kati ya Kenya na Madagascar, mechi itakayopigwa Uwanja wa Moi.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF), lilitoa nafasi kwa nchi hizo za Afrika Mashariki, kuandaa michuano hiyo ya CHAN ili kuzipa uzoefu kabla ya kufanyika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2024, zitakazofanyika mwakani kwa ushirikiano wa mataifa hayo matatu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED