Azam: Hatutaki kombe, tunahitaji kujenga timu

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 12:10 PM Aug 20 2025
news
Picha Mtandao
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Azam, Thabit Zacharia.

UONGOZI wa Azam FC umesema ushiriki wao katika mashindano maalum yanayoendelea huko Rwanda ni kwa ajili ya kumpa nafasi kocha wao, Florent Ibenge, kukijenga kikosi kabla ya kuanza kwa msimu mpya.

Akizungumza na Nipashe jana kutoka Rwanda, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Azam, Thabit Zacharia 'Zaka', alisema mashindano hayo maalum ya maandalizi ya msimu mpya yaliyoandaliwa na APR, yatawapa nafasi ya kuona uimara na mapungufu ya timu yao.

Ofisa huyo alisema wanaamini kupitia michuano hiyo, kikosi chao kitapata michezo mingi ya kirafiki ambayo itawasaidia kuwapa uzoefu wachezaji wao ili kukabiliana na ushindani unaotarajiwa kwenye msimu mpya wa mashindano.

"Hatuchezi michezo yetu huku kwa ajili ya kombe, kama itatokea tumepata kombe ni sawa lakini tupo huku Rwanda kwa ajili ya kuandaa timu, kumpa kocha wetu nafasi ya kupima kikosi chake pamoja na kujaribisha mifumo yake," alisema Zaka.

Aidha, alisema kama kocha ataona mapungufu yoyote awe na muda wa kuyafanyia kazi kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa watakayoshiriki.

"Msimu huu tutashiriki kombe le Shirikisho Afrika na droo yake imeshachezeshwa, huu ni wakati wa kuandaa timu yetu, kocha aangalie nini cha kuongeza, kama itatokea tumeshinda mechi zote na kuchukua kombe sawa, lakini sio kipaumbele chetu," alisema Zaka.

Michuano hiyo ya APR Pre Season iliyoanza juzi inashirikisha timu nne ambazo ni pamoja na Azam, Power Dyanamos ya Zambia, Polisi FC, AS Kigali na wenyeji APR ambao walianza michuano hiyo kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Power Dynamos.

Michuano ya mwaka huu ya Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC wamepangwa kuanza hatua ya awali kwa kucheza dhidi ya El Merreikh ya Sudan.