LICHA ya kocha Fadlu Davids, kusifu usajili uliofanyika, bado amesema anahitaji mshambuliaji mmoja mwenye uwezo wa kufanya maamuzi binafsi mbele ya lango la pinzani.
Akizungumza kutoka nchini Misri mara baada ya kumalizika mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Wadi Degla SC ya nchini humo uliochezwa juzi, Fadlu, alisema msimu unaokuja watahitaji kufanya vyema kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na kuwapita wapinzani wao Yanga, hivyo wanahitaji mshambuliaji wa maamuzi binafsi yenye faida kwa timu.
"Unakumbuka baadhi ya mechi ngumu msimu uliopita tulikuwa tunakosa mchezaji mkubwa ambaye anaweza kukupa kitu, anaweza kuamua mchezo mkubwa, mfano mechi kama ya fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya RS Barkane ya Morocco, dhidi ya Yanga tulikuwa tunakosa mchezaji kama huyo," alisema Fadlu.
Anasema wanahitaji mshambuliaji huyo ambaye anaweza kuibeba Simba Sports mgongoni kwake mambo yanapokuwa magumu uwanjani.
"Bado kuna siku kabla ya dirisha la usajili kufungwa, wana uwezo wa kupata aina hiyo ya mchezaji ili kukamilisha kikosi kabla ya kuanza msimu mpya wa mashindano," alisema Fadlu.
Aidha, alisema suala hilo analiacha mikononi mwa Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohamed Dewji na wadhamini wa klabu chini ya Mkurugenzi wake, Joseph Rwegasira, ambao wanaweza kufanikisha usajili huo.
Akizungumzia mchezo wa juzi ambao Simba ilishinda mabao 2-0, yaliyofungwa na Elie Mpanzu na Kibu Denis, kocha huyo raia wa Afrika Kusini alisema walicheza vyema, lakini wangeweza kupata ushindi mkubwa zaidi kama wachezaji wake wangekuwa makini.
"Tumecheza vyema, tungeweza kufunga mabao mengi kwenye mchezo huu, lakini tumefurahi kwa kile tulichokipata," alisema.
Kikosi cha timu hiyo kinatarajiwa kuwasili hapa nchini leo baada ya kuwa Misri tangu Julai 30 kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa mashindano.
Mbali na kambi, imecheza michezo minne ya kirafiki, ikishinda mitatu na kupoteza mmoja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED