KWA mara ya kwanza, Klabu ya Azam, imefunguka juu ya sakata zima la kiungo mshambuliaji wake, Feisal Salum, ikisema hakuna klabu yoyote ya ndani iliyopeleka ofa, wala yeye mwenyewe kuomba kuondoka, kabla ya kuamua kumwongeza mkataba wa mwaka mmoja.
Azam imesema mkataba huo utamfanya alipwe mshahara mkubwa zaidi kuliko wachezaji wote wa ndani na nje ya nchi wanaocheza soka hapa nchini.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo, Abdulkarim Amin 'Popat', alisema licha ya kwamba kuna klabu moja kutoka nje ya nchi ilikuwa inamhitaji, lakini ikashindwa kufikia dau waliloliweka, ila hakuna timu yoyote hapa ichini iliyofanya hivyo, zaidi ya kusikia kwenye mitandao ya kijamii na tetesi za usajili.
"Sakata la Fei Toto halikuwa rahisi kihivyo, lakini wala halikuwa na ugumu kama vile lilivyokuwa likiripotiwa na mitandao ya kijamii pamoja na tetesi mbalimbali. Fei Toto hakuwahi kutufuata hata siku moja kutuambia kama anataka kuondoka, kuna klabu moja kutoka nje ya nchi ilimhitaji, lakini yeye mwenyewe hakuwahi kutamka kuwa anataka kuondoka kama inavyozungumzwa," alisema.
Popat alisema kilichokuwapo ni Fei Toto kuchelewa kusaini mkataba uliopo mezani kitu ambacho ni kawaida kwa mkataba wowote ule.
"Kilichokuwapo mezani ni mkataba ambao yeye alikuwa hajausaini na watu wanashindwa kuelewa kuwa huu ni sawa na mikataba mingine ya kazi, ni lazima pande zote mbili ziridhie ndipo usainiwe, ni makubaliano ya pande zote mbili, kama kuna vipengele hamjakubaliana hauwezi kusainiwa," alisema.
Hata hivyo, alisema tayari mchezaji huyo ameshasaini mkataba wenye maboresho makubwa utakaomfanya kubaki kwenye viunga vya Chamazi hadi 2027.
"Leo naweza kuzungumza rasmi kuwa suala hili limekwisha, ameongeza mkataba wa mwaka mmoja, ule wa mwanzo ulikuwa unaisha 2026, lakini huu unamfanya kukaa Azam hadi 2027.
"Ni mkataba wenye maboresho mazuri zaidi ya ule wa mara ya kwanza ambao unamfanya awe mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwa wachezaji wote wanaocheza soka la Tanzania, awe mzawa au mchezaji anayetoka nje ya nchi," alibainisha ingawa hakuweka wazi kiasi cha mshahara wa mchezaji huyo atakaokuwa analipwa.
Awali iliripotiwa kuwa Klabu ya Simba, Yanga na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini zilikuwa zinamhitaji mchezaji huyo, ambapo zilienda mbali zaidi zikidai zilikuwa tayari kununua mkataba wake ili aondoke klabuni hapo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED