FIFA, CAF wampongeza Karia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:33 PM Aug 20 2025
news
Picha Mtandao
Rais mteule wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF) Wallace Karia.

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino na Rais wa (CAF), Patrice Motsepe, wamempongeza, Wallace Karia, kwa kuchaguliwa tena kuliongoza shirikisho la soka hapa nchini (TFF).

Infantino katika salamu zake za pongezi amemtakia mafanikio Karia pamoja na Kamati ya Utendaji ya TFF iliyochaguliwa kutimiza vyema majukumu yao kwa muda wa miaka minne watakayokaa madarakani.

Rais huyo amemshukuru Karia kwa juhudi, kazi na mchango wake muhimu katika maendelea ya mpira wa miguu pamoja na kusimamia thamani yake.

Motsepe amesema anampongeza Karia kwa kuchaguliwa tena na anaahidi CAF itaendelea kutoa ushirikiano kwa uongozi huo mpya uliochaguliwa Jumamosi iliyopita.

"Kuchaguliwa kwako tena ni ishara ya imani ya wanachama wako kwa uongozi wako bora, najivunia sana bidii yako na kujitolea kwa maendeleo na ukuaji wa soka la Tanzania," alisema Motsepe.

Kiongozi huyo ameitaka Kamati ya Utendaji ya TFF iliyochaguliwa kuendelea kusaidia maendeleo ya mpira wa miguu kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Mbali na Karia, viongozi wengine waliosajiliwa ni pamoja na Athumani Nyamlani ambaye alishinda tena cheo cha Nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Nassor Idrissa (Makamu wa Pili wa Rais) huku wajumbe wakiwa ni pamoja na Khalid Mohamed, Issa Bukuku, Mohamed Aden, James Mhagama na Somoe Ng'itu.

Wajumbe wengine ni Salum Kulunge, CPA Hossea Lugano, Debora Mkemwa, Azzan Mufti na Evance Mgeusa.