Kilimanjaro Sweden yatwaa ubingwa bonanza Ubelgiji

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 04:24 PM Aug 17 2025
Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi (kushoto) na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Jestas Nyamanga, wakimkabidhi kombe la ubingwa wa Bonanza la Serengeti nahodha wa timu ya Kilimanjaro kutoka Sweden, Abbas Bachu.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mobhare Matinyi (kushoto) na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Jestas Nyamanga, wakimkabidhi kombe la ubingwa wa Bonanza la Serengeti nahodha wa timu ya Kilimanjaro kutoka Sweden, Abbas Bachu.

TIMU ya soka ya Watanzania Kilimanjaro kutoka Sweden imetwaa tena kwa mara ya nne mfululizo ubingwa wa kombe la Bonanza la Serengeti katika michuano iliyofanyika Agosti,15-16 mwaka huu jijini Antwerp Ubelgiji.

Kilimanjaro ilitetea ubingwa huo baada ya kuifunga timu nyingine ya Watanzania kutoka Uingereza iitwayo Leeds Swahili kwa ushindi wa mabao 2-1 kwenye mchezo mkali wa fainali.  Magoli ya Kilimanjaro yalifungwa na Feisal Amir na Fryad Sabri huku la Leeds likifungwa na Murtaza Fuad. Hii ni mara ya tatu kwa timu hizi kukutana fainali.

Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Jestas Nyamanga, alimkabidhi kombe la ubingwa nahodha wa Kilimanjaro, Abbas Bachu, ambaye naye alimkabidhi Balozi wa Tanzania nchini Sweden,  Mobhare Matinyi, na kuibua shwange za washabiki wao.

Kilimanjaro hushiriki ligi ya daraja la sita nchini Sweden katika mfumo wa madaraja saba.

Michuano hiyo iliyofanyika kwa mara ya nne tangu mwaka 2021 na huandaliwa kwa lengo la kuwaunganisha Watanzania Ughaibuni, kukuza vipaji vya soka na kuitangaza nchi kimataifa. 

Mtanange huo ulishuhudiwa na Mkurugenzi wa Diaspora kutoka Tanzania, Salvatory Mbilinyi, Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Caroline Chipeta na Mabalozi wa Kenya, Sudan Kusini na Somalia nchini Ubelgiji.

Katika mtanange huo, jumla ya timu 15 za watanzania na watu wa Afrika Mashariki waishio barani Ulaya zilimenyana. Waandaaji Tanzania walikuwa na timu kumi kutoka Sweden, Ubelgiji, Uholanzi, Uingereza, Scotland, Ujerumani na Ufaransa huku Burundi ikiwa na timu tatu na moja moja kutoka Rwanda na Somalia.