UONGOZI wa klabu ya KMC, umesema kocha wao mpya, Marcio Maximo, anataka timu hiyo imalize angalau kwenye 'Top 4' Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Akizungumza jana Jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Khalid Chukuchuku, alisema hiyo inamfanya kocha huyo raia wa Brazil, kukitengeneza kikosi cha ushindani ili kufikia lengo lake hilo.
Alisema katika maandalizi yanayoendelea , maximo anakitengeneza kikosi cha ushindani chenye uwezo wa kupambana na timu yoyote kwenye ligi.
"Kocha wetu Maximo, anaendelea na mazoezini, tunaelekea wiki ya nne ya 'Pre seasons', tunaendelea vizuri sana, tunaamini mafunzo ya mwalimu wetu mpya chini ya Maximo yatakifanya kikosi kiwe bora zaidi, wachezaji wetu wapya wameshaanza kuzoea mazingira, wameshazoeana na wenzao, mpaka kufikia wiki ya mwisho kabla ya kuanza Ligi, tutakuwa tayari kwa mikikimikiki," alisema Chukuchuku.
Kuhusu malengo ya msimu ujao, alisema kocha wao amewaambia kikosi alichonacho kinaweza kumaliza ndani ya nne bora na hayo ndiyo malengo yao ya juu kuelekea msimu ujao.
"Tumepania kweli kweli kuelekea msimu ujao, unajua msimu uliopita haukuwa mzuri sana kwetu kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kubadilisha makocha mara kwa mara, lakini sasa tumejidhatiti angalau tumalize nafasi nne za juu na Maximo ameshatuambia kwa kikosi alichonacho, ukichanganya na uwezo, uzoefu wake kinaweza kabisa kushika nafasi hiyo na kucheza mechi za kimataifa msimu ujao," alisema Chukuchuku.
KMC, imerejea Dar es Salaam siku chache zilizopita kutoka mjini Zanzibar, ilipokwenda kuweka kambi ya wiki mbili ya maandalizi ya msimu ujao.
Mafanikio ya juu kabisa kwa KMC yalikuwa ni 2019, ilipofanikiwa kucheza Kombe la Shirikisho, ingawa ilitolewa hatua ya awali na AS Kigali, licha ya kulazimisha suluhu ugenini, Agosti 10 mwaka huo, ilifungwa mabao 2-1 nyumbani, Agosti 23.
Msimu uliopita ilishika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ilipokusanya pointi 35.
Msimu ujao itakuwa chini ya Maximo, aliyewahi kuifundisha timu ya taifa 'Taifa Stars', 2006 hadi 2010, kabla ya kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, mwaka 2014.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED