KLABU ya Namungo imeweka rekodi ya kuacha wachezaji wengi zaidi kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu.
Namungo imeacha jumla ya wachezaji 13, ikifuatia na Pamba Jiji ambayo imeachana na wachezaji 11.
Kwa Namungo imeachana na wachezaji ambao haiwahitaji tena kwa msimu ujao wa Ligi Kuu, wengine wakiwa wanarudi kwenye klabu zao baada ya kumaliza mkopo pamoja na kuuza.
Klabu imemuuza beki wa pembeni Antony Mlingo kwenda Simba, huku pia ikimwachia Salehe Karabaka aliyekuwa akicheza kwa mkopo akitokea Wekundu wa Msimbazi kurejea.
Wachezaji wengine walioachwa ni Beno Kalolanya, aliyekwenda kujiunga na Mbeya City, Emmanuel Asante, Erasto Nyoni, Meddie Kagere, Erick Malongi, Derick Mukombozi, Issa Abushehe, Joshua Ibrahim na Erick Kapaito. Wengine ni Emmanuel Charles, na Anderson Solomoni.
Kwa sasa Namungo iko kwenye harakati za kufanya usajili ambao utairudisha kwenye chati ya msimu takriban mitatu au minne iliyopita ambapo ilikuwa timu tishio kwenye Ligi Kuu.
Katika kujiimarisha inaelezwa tayari imesajili wachezaji kadhaa, akiwamo Heritier Makambo, straika wa zamani wa Yanga, aliyeichezea Tabora United msimu uliomalizika.
Nayo Pamba jiji FC, imekuwa timu ya pili kuwapa 'thank you', wachezaji kuelekea msimu ujao wa mashindano.
Timu hiyo imesafisha wachezaji kadhaa ambao ni Christopher Oruchum, Ladry Bakari, Deusa Kaseke, Ally Ramadhani 'Oviedo', Paul Kamtewe, Mwaita Gereza na Abalkassim Suleiman.
Wachezaji wengine waliopewa mkono wa kwaheri na Pamba Jiji ni Cherif Ibrahim, George Mpole, Ibrahim Isihaka, Modou Camara na Lazaro Mlingwa.
Tayari timu hiyo imetangaza kumsajili mfungaji bora wa Ligi Kuu Zanzibar msimu uliomalizika, Abdallah Idd Pina, huku ikithibitisha kumpokea kiungo mkabaji, Kelvin Nashon kutoka Singida Black Stars aliyepelekwa kwa mkopo.
Pamba Jiji imeshatangaza baadhi ya wachezaji ambao wamewasajili akiwamo Hassan Kibailo, aliyerejea tena kikosini akitokea Namungo FC, Amos Kadikilo kutoka Fountain Gate.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED