Simba nguvu moja

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 01:47 PM Apr 20 2025
Wachezaji wa Simba wakifanya mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya kwanza ya hatua ya nusu fainali ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch kutoka Afrika Kusini itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa New Amaan Comple
Picha: Simba SC
Wachezaji wa Simba wakifanya mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mechi ya kwanza ya hatua ya nusu fainali ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stellenbosch kutoka Afrika Kusini itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa New Amaan Comple

SIMBA inatarajia kuikaribisha Stellenbosch FC kutoka Afrika Kusini katika mechi ya kwanza ya hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa leo kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar huku ikipania kurejea ilichofanya mwaka 1993 katika michuano hiyo ya kimataifa ya CAF.

Wawakilishi hao pekee wa Afrika Mashariki waliobakia katika michuano ya kimataifa waliiondoa Atletico Sport Aviacao ya Angola na kufanikiwa kutinga  fainali.

Imepita miaka 32 kwa Simba kushindwa kutinga nusu fainali ya michuano ya kimataifa na badala yake kuishia robo fainali kwa misimu sita, mwaka huu imepania kuvunja rekodi yake.

Katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam (sasa Uhuru), Simba iliifunga Atletico Sport Aviacao mabao 3-1, mawili yakifungwa na Edward Chumila na Malota Soma akifunga moja, huku Nelo Miguel, akiwafungia Waangola bao la kufutia machozi.

Katika mchezo wa marudiano uliochezwa Luanda, Angola, ambao Watanzania wengi walikuwa na mashaka kama inaweza kuvuka kutokana na uwezo mkubwa walioonyesha wachezaji wa timu hiyo kwenye mchezo wa Dar es Salaam licha ya kupoteza, ikiwa na kina Kanka Vemba, Abilio Amaral, Lolo, Yanda, kapteni Bravo da Rosa, Simba ililazimisha suluhu na  nyota wa mchezo akiwa ni golikipa namba moja wa Mnyama na Tanzania (Taifa Stars), Mohamed Mwameja.

Safari hii, Simba imeingia hatua hiyo kwa kuiondosha Al Masry ya Misri kwa penalti 4-1, baada ya kila timu kushinda mabao 2-0 nyumbani, wakati wapinzani wao wametinga hatua ya nusu fainali kwa kuwavua taji mabingwa watetezi, Zamalek ya Misri, ikitoka suluhu nyumbani Afrika Kusini, kabla ya kwenda kushinda bao 1-0 ugenini.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema kila kitu kimekwenda kama kilivyopangwa, kilichobaki ni dakika 90 za uwanjani, zitakazotekelezwa na wachezaji wake.

Fadlu alisema wamefanya kila kitu ikiwa kusoma mbinu za wapinzani wao ambazo wanazifahamu na kuziingiza katika vichwa na miguu ya wachezaji wake ili kuzuia hatari zao pamoja na kutumia udhaifu wa timu hiyo kuwaadhibu.

"Wimbo ni mmoja tu, kushinda ili kujiweka katika mazingira mazuri kuelekea mchezo wa marudiano huko Durban, hatutaki kwenda huko tukiwa na wasiwasi sana, kikubwa ambacho nimesisitiza ni kutoruhusu bao ambalo kwao litakuwa la ugenini, ili isiende kutupa shida na wakati mgumu ugenini," alisema Fadlu.

Naye mlinzi wa kati wa Stellenbosch, Brian Mandela Onyango, raia wa Kenya, amekiri  Simba ni timu bora na wachezaji wao watakuwa tishio katika mchezo huo wa leo.

Onyango amesema hao wamejiandaa kikamilifu kukabiliana nao katika mechi hiyo ya nusu fainali ili kujiweka kwenye nafasi ya kusonga mbele.

"Tumejiandaa na kila kitu kipo tayari, tunajua tunakabiliana na timu ambayo iko vizuri, imekuwa katika mashindano haya kwa miaka mingi na ina wachezaji wanaojua wanachokifanya," alisema Onyango.

Katika kuhamasisha kupata ushindi, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kutoka Sh. milioni 20 kwa kila bao litakalofungwa na Simba endapo watapata ushindi.

"Watanzania wote tuwaombee dua Simba, ni mechi muhimu dhidi ya Stellenbosch kule Zanzibar, ni mechi muhimu ya kufa na kuona kwa Tanzania, Serikali, Dk. Samia Suluhu Hassan, anawatakia kila la heri, tunahitaji kuwaombea, goli la mama katika nusu fainali ni Sh. milioni 20, mzigo wa fainali tutautangaza baada ya kuvuka fainali, lakini kila la kheri Simba, ni muhimu kwa taifa," Gerson Msigwa, Msemaji wa Serikali, amesema.

Aliongeza motisha kwa ajili ya hamasa ya hatua ya fainali itatangazwa baadaye.