WAKATI klabu ya Simba ikitangaza rasmi kumuuza straika wake raia wa Cameroon, Leonel Ateba, imetamba kuwa kwa usajili mkubwa walioufanya msimu huu watamaliza unyonge wao wa kutopata taji lolote nchini kwa misimu minne, huku pia ikisema lengo lao kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika usimu ujao ni kufika nusu fainali.
Akizungumza jana kutoka jijini Mbeya, alipokwenda kufungua matawi ya klabu hiyo, Meneja Habari wa Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema hawatokubali tena kwa msimu huu, na hilo wameanza kulifanya kwa vitendo baada ya kusajili wachezaji bora na wenye viwango vya hali ya juu kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.
"Huu ni msimu wa Simba. Ni msimu ambao tumejiandaa, tumejidhatiti na tumejipanga kwenda kufanya vizuri. Kwa miaka minne tumekuwa tukiishi kinyonge sana kutokana na kutofanya vyema, hasa kwenye ligi ya ndani, tumepoteza mataji yote, hii siyo hali nzuri kwa klabu kama ya Simba.
“Ndiyo maana msimu huu tumefanya usajili bora, tumechukua wachezaji wazuri, wenye viwango na uwezo wa hali ya juu, tumechukua nyota kutoka Afrika Kusini kwenye klabu kubwa ya Mamelodi Sundowns.
“Tunatambua uwezo na uzoefu wao, watakuja kutufanyia kazi iliyotukuta, tunawaambia wanachama na mashabiki wa Simba, msimu huu unyoge basi. Ni mwaka wa Simba kurejesha heshima yake," alitamba Ahmed.
Alisema pamoja na kusajili wachezaji wapya, lakini wamehakikisha wanawabakisha wachezaji wote ambao wanahitajika kwenye kikosi kwa kuwaongezea mikataba
"Wachezaji wote wazuri ambao tulitaka kuendelea nao tumewaongeza mikataba. Ni msimu wa Simba kurejesha heshima na mataji yote na Wanasimba kufurahi.
“Kuhusu maendeleo ya timu ni mazuri tangu tumeweka kambi yetu nchini Misri, tumekuwa na kambi bora, jambo linalotupa faraja ni kitendo cha kupambana na kubakisha Kocha Mkuu, Fadlu Davids ambaye alikuwa anatakiwa na klabu mbalimbali kubwa barani Afrika," alisema.
Ahmed alisema kwenye michuano ya kimataifa, malengo ya Simba msimu ujao ni kufika hatua ya nusu fainali.
"Hayo ndiyo malengo yetu mama, kama tukivuka hapo, kufika fainali na kutwaa ubingwa itakuwa ni jambo bora, lakini tunataka tufikie hapo kwenye nusu," alisema.
Wakati huo huo, klabu hiyo imetangaza kuondoka kwa straika wao, Ateba, aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu uliopita akitokea USM Alger ya Algeria.
"Asante Ateba kwa muda wote uliokuwa sehemu ya kikosi chetu." iliandikwa sehemu ya taarifa ya klabu hiyo.
Mchezaji huyo ameuzwa kwa klabu ya Al Shorta ya Iraq kwa Sh. Milioni 740.
Ateba atashiriki Ligi ya Mabingwa barani Asia ambapo timu yake hiyo mpya inashiriki.
Wakati hayo yakiendelea, wasifu wa straika wa Wydad Casablanca, Selemani Mwalimu umebadilika kwenye mitandao ya kijamii, ambapo kwa sasa unasomeka kama mchezaji wa Simba.
Pia mtandao wa mashabiki wa Wydad Casablanca, umeandika kwa lugha ya Kiarabu kuwa; "Kuna makubaliano ya mwisho kati ya klabu ya Wydad Athletic na Simba ya Tanzania kuhusu kumwazimisha mshambuliaji Suleiman kwa mkopo," uliandikwa mtandao huo wa mashabiki wa klabu hiyo kwa lugha ya Kiarabu.
Ingawa klabu ya Simba haijasema jambo lolote kuhusu mchezaji huyo, lakini habari zinasema kila kitu kimekamilika kwa mchezaji huyo wa Kitanzania, aliyesajiliwa na Wamorocco kutoka Fountain Gate, kinachosuburiwa ni kutangazwa tu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED