KATIKA kuhakikisha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, inafanya vizuri kwenye mchezo wake wa robo fainali dhidi ya Morocco, serikali imepokea hundi ya Sh. milioni 30 kutoka Benki ya Biashara ya NMB kwa ajili ya kununua tiketi za mashabiki pamoja na motisha kwa wachezaji.
Taifa Stars, ambayo imeongoza Kundi B la michuano ya Wachezaji wanaocheza Soka la Ndani Afrika (CHAN), Ijumaa itavaana na Morocco katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, majira ya saa mbili usiku, ukiwa ni mchezo wa robo fainali ya mashindano hayo.
Morocco imemaliza katika nafasi ya pili kwenye Kundi A, lililokuwa likizijumuisha pia mwenyeji Kenya, ambayo ni kinara wa kundi hilo, DR Congo, Angola na Zambia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, wakati alipokuwa akikabidhiwa fedha hizo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, aliishukuru benki hiyo kutokana na fedha walizozitoa wakiwa na lengo la kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwenye sekta ya michezo.
"Tunaishukuru Benki ya NMB kwa fedha ambazo wamezitoa kwa lengo la kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya michezo kuhakikisha timu yetu ya taifa inaingia hatua ya fainali katika mashindano ya CHAN," alisema Msigwa.
Aliziomba pia taasisi nyingine zijitokeze kuiunga mkono timu ya taifa ili iweze kupata matokeo mazuri katika mchezo huo wa robo fainali.
Aidha, aliwataka Watanzania wajitokeze kwa wingi uwanjani kwa ajili ya kuisapoti timu hiyo kwa kujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Donatus Richard, ambaye ni mwakilishi kutoka NMB, alisema miongoni mwa fedha walizozitoa Sh. milioni 20 ni kwa ajili ya kununua tiketi za mashabiki na Sh. milioni 10 ni motisha kwa wachezaji.
"Tumeamua kutoa fedha hizi kwa ajili ya kuhakikisha mashabiki wanajaza uwanja Ijumaa pamoja na kuwapa motisha wachezaji ili kufanya vizuri katika mchezo huo," alisema Richard.
Ally Kamwe, mhamasishaji wa Taifa Stars ambaye pia ni Msemaji wa Yanga, aliipongeza timu hiyo kwa kufanikiwa kuingia hatua ya robo fainali bila kupoteza mchezo hata mmoja.
"Tuna kikosi kizuri ambacho ninaamini Ijumaa kitatupa heshima kwa kuifunga Morocco kwani huu ni mwaka wa kuleta kombe nyumbani," alisema Kamwe.
Alisema Jumatano wiki hii wataanza kufanya hamasa rasmi ya mchezo huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED