TANZANIA imepangwa kundi A katika Mashindano ya Kombe la Dunia ya mchezo wa Kabbadi ya ufukweni, ikiwa na timu za Malaysia, Hungary na China.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza Septemba 23 hadi 29 mwaka huu kwenye fukwe za Port Dickson nchini Malaysia.
Akizungumza na Nipashe jana, Mwenyekiti wa Chama cha mchezo wa Kabbadi Tanzania (TSA), Abdalah Nyoni baada ya kupangwa kwa makundi hayo, wachezaji wanaendelea na mazoezi ili kujiweka fiti zaidi.
"Kwa sasa timu zinaendelea na mazoezi katika Viwanja vya Mwembe Yanga kuhakikisha zinakwenda kufanya vizuri katika mashindano hayo, ambayo yanatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa," alisema Nyoni.
Alisema malengo ni kuona timu zinafanya vizuri kwa kupata ushindi katika michezo yao yote watakayoicheza.
Alisema kambi rasmi itaanza Septemba 8 mwaka huu kwenye Chuo Kikuu cha Kimataifa Kampala kilichopo Gongo la Mboto, Dar es Salaam.
Alisema timu itaondoka Septemba 23 na kuomba wadau wajitokeze kuwasaidia viongozi na wachezaji posho kwa ajili ya matumizi binafsi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED