TIMU ya Soka ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), imebakiza dakika 180 ili kufuzu kwa mara ya pili mfululizo kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (WAFCON 2026), baada ya kuiondoa Equatorial Guinea.
Ikiwa ugenini, Twiga Stars imesonga mbele katika mashindano hayo baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Equatorial Guinea, kwenye mechi ya michuano hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Malabo, juzi jioni na kufanya ushindi wa jumla kuwa mabao 4-2.
Twiga Stars sasa itacheza raundi ya pili na ya mwisho dhidi ya Ethiopia hapo Oktoba, mwaka huu baada ya wapinzani hao kuondoka Uganda.
Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Bakari Shime, amewapongeza wachezaji wake kwa kupambana katika mechi hiyo na kumalizika kazi waliyoianza nyumbani wiki iliyopita.
"Mechi ilikuwa ngumu sana, pia hali ya mvua kubwa iliyonyesha ilitusumbua, ila katika maisha yangu ya soka hii ndio ilikuwa mechi ambayo tumepigiwa faulo nyingi sana, nirudie kusema nawapongeza sana wachezaji wangu, tunarudi nyumbani kwa ajili ya kujipanga kukutana na Ethiopia," alisema Shime.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Mkuu wa Msafara, Sarah Chao, aliliambia gazeti hili haikuwa kazi rahisi kuwaondoa wapinzani wao.
"Tunamshukuru Mungu kwa kusimama na sisi, ilikuwa ni mechi ngumu sana kwa kila upande," alisema kwa kifupi Chao.
Aliongeza kikosi cha Twiga Stars kinatarajia kurejea nyumbani leo alfajiri.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED