Vita ya namba Simba yaanza kambini Misri

By Adam Fungamwango ,, Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 12:08 PM Aug 27 2025
news
Picha Mtandao
Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu.

MENEJA wa Simba, Patrick Rweyemamu, amebainisha kuwa kumekuwa na vita kali ya kuwania namba kwa wachezaji wapya waliosajiliwa, huku akitabiri kuna uwezekano wa idadi kubwa ya wachezaji wapya wanaweza kuingia kwenye kikosi cha kwanza msimu ujao.

Akizungumza jana kutoka nchini Misri, Rweyemamu pia amesema usajili wa wachezaji wapya kwa kikosi hicho bado haujakamilika ambapo baadhi yao wataungana nao wakisharejea jijini Dar es Salaam.

Simba iko nchini Misri tangu Julai 30, mwaka huu, ambapo imekwenda kuweka kambi kwa ajili ya msimu mpya wa mashindano kama ilivyofanya msimu uliopita.

"Niseme tu kuwa huku kuna vita, kuna vita kweli kweli ya kuwania namba, mazoezini kunachimbika, ukiangalia kikosi chetu cha msimu uliopita hatujakibadilisha sana, tuna wachezaji kama watatu tu wanne ambao hawatokuwapo, lakini walikuwa sehemu ya kikosi cha kwanza msimu uliopita.

"Lakini kwa mazoezi ninavyoyaona na wachezaji wapya waliosajiliwa wanavyoleta chachu, kuna uwezekano mkubwa kikosi cha kwanza kikaundwa na nusu ya wachezaji wa zamani na wengine nusu ya pungufu kidogo kikatokana na wachezaji wapya," alisema meneja huyo.

Alisema kwenye mazoezi ya timu hiyo, wachezaji wengi wapya wameleta chachu kubwa kiasi hata cha kuwafanya hata wale waliokuwa wanakosa namba msimu uliopita nao kuchangamka.

"Wachezaji wengi waliosajiliwa msimu huu, wamekuja kuleta chachu, wamekuja kuleta ushindani, wamekuja kuhakikisha kuwa si kwamba wanaweza kupambania namba, bali kuzichukua kabisa.

"Unaweza kuwa msimu bora zaidi kuliko mingi iliyopita kwa Simba kwa sababu wigo wa upana wa kikosi umeongezeka, tuna wachezaji ambao wametoka kwenye timu ambazo huko walikuwa si tu kama wanacheza, bali ni tegemeo, naamini wanakuja kutupa kitu bora na msimu unaokuja tutakuwa bora zaidi kuliko misimu mingi iliyopita," alisema Rweyemamu.

Akizungumzia usajili alisema anachofahamu ni kwamba usajili bado unaendelea na baadhi ya wachezaji wapya wataungana nao watakaporejea jijini Dar es Salaam, kesho.

"Yaani wachezaji wetu wapya wanaweza kufika hata 12, wengine walikuwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa, Taifa Stars kwenye michuano ya CHAN, wapo ambao hawakuwa kwenye kikosi, lakini tumewasajili na tutaungana nao tukishafika huko," alisema.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Kitengo cha Habari cha klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema wamefanya usajili wa matakwa ya kocha ili kuhakikisha wanafanya vizuri.

"Usajili huu tuliofanya unatupa matumaini makubwa sana, kocha wetu ameufurahia kwa sababu tumefanya kile ambacho alikipendekeza katika maboresho," alisema Ahmed.

Aidha, alisema msimu ujao watakuwa makini zaidi na kutoruhusu makosa yoyote yatakayowafanya wasifikie malengo yao.

"2025/26, huu ni msimu wetu, Simba tumejiandaa, tumejipanga na tumejidhatiti haswa kufanya vizuri, mashabiki na viongozi tumeteseka kwa miaka minne kukosa ubingwa, hii si kawaida yetu, tunaenda kurudisha ufalme wetu."

"Wachezaji wote wazuri ambao tulitaka kuendelea nao tumewaongeza mikataba, ni msimu wetu kurejesha heshima na mataji yote kuhakikisha mashabiki wanakuwa na furaha tena,” alisema.