WACHEZAJI wapya watatu waliotangazwa hivi karibuni, Issa Fofana, Baraket Hmidi na Ben Zitoune Tayeb, wameahidi kuipa Azam FC mataji msimu ujao.
Wakizungumza wakiwa kwenye maandalizi ya timu hiyo kuelekea msimu mpya wa mashindano, wachezaji hao wamewaambia mashabiki wa Azam kuwa kipindi cha ukame wa mataji kimekwisha kwani wamekuja kupambana kuhakikisha klabu hiyo inafikia malengo yake iliyojiwekea pamoja na kutwaa mataji.
Fofana, raia wa Ivory Coast, anayecheza nafasi ya golikipa, amesajiliwa kutoka Al Hilal ya Sudan, Baraket raia wa Tunisia, alikuwa akiichezea CS Sfaxien, huku Zitoune pia raia wa Tunisia, amejiunga nayo akitokea Al Hilal.
"Nina furaha sana kujiunga na Azam , nawaahidi nitawapa kile ambacho klabu imefikiria kunisajili, nitafanya kila kitu kuhakikisha inashinda michezo na mataji, nina furaha sana kuwapo hapa Tanzania, hii ni historia kubwa sana kwangu, nadhani mashabiki wa timu hii watakuwa na msimu mzuri sana," alisema Baraket anayecheza nafasi ya winga.
Zitoune, alisema amekubali kujiunga na Azam kwa sababu ni moja kati ya timu kubwa Afrika kwa sasa, hivyo ataitumikia kwa nguvu na ujuzi wake wote kuhakikisha timu inapata mataji msimu huu.
"Nina furaha kujiunga na Azam, moja ya timu kubwa Tanzania, nawaahidi mashabiki kuwa nitaitumikia kwa nguvu na ujuzi wangu wote ili tupate ushindi na mataji pamoja na kufikisha malengo yote ya klabu," alisema Zitoune ambaye ni beki.
Fofana, golikipa wa timu hiyo alisema amemshukuru kila mmoja aliyehakikisha anatua kwenye klabu hiyo, akiahidi lango la Azam litakuwa salama muda wote
"Napenda kumshukuru kila mmoja, naahidi nitalilinda lango la Azam, lengo ni kuipa timu ushindi na mataji pia kwa msimu ujao wa mashindano yote," alisema Fofana.
Azam imefanya usajili mkubwa msimu huu, ambao umeonekana kulenga zaidi mechi za kimataifa, ikijiandaa kucheza Kombe la Shirikisho Afrika.
Timu hiyo imepangwa kucheza dhidi ya El Merriekh FC Bentiu ya Sudan Kusini, Septemba 19, mchezo wa hatua za awali utakaochezwa ugenini, kabla ya marudiano hapa nchini, Septemba 26, mwaka huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED