WATANZANIA wametakiwa kuondoa dhana potofu kuhusu mchezo wa gofu kwamba unachezwa na matajiri, bali ni wa watu wote na kwa rika lolote, huku wazazi na walezi waombwa kuwaruhusu watoto wao hususani wa kike kujifunza.
Kauli hiyo imetolewa na Meja Jenerali, Wilbert Ibuge juzi katika viwanja vya Klabu ya Gofu Lugalo, Dar es Salaam, wakati akifunga mashindano ya mchezo huo yaliyopewa jina la 'maisha ni hesabu'.
Mashindano hayo yalishirikisha wachezaji mbalimbali, ambapo mshindi ataiwakilisha nchi katika mashindano ya kikanda ya Afrika Mashariki, Novemba mwaka huu.
"Kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi, Jenerali John Mkunda nipo hapa kumwakilisha katika utoaji wa tuzo hizi. Tuzo hizi ni namna ya kukuza vipaji kwa vijana wadogo wanaojifunza gofu. Washindi wengine wataenda Nairobi kwa ajili ya kushiriki mashindano ya kikanda," alisema Jenerali Mkunda.
Hivyo, aliwaomba Watanzania kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika kukuza vipaji vya wachezaji wa mchezo wa gofu.
Alisema mchezo huo ni sehemu ya vijana kujifunza na kuwa wataalamu pamoja na kupata ajira na ujuzi katika maisha yao.
Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya washindi wa shindano hilo, Nsajigwa Mwansasu ambaye ni kepteni wa timu ya JWTZ gofu Klabu alisema: "Nimejupanga vizuri, nitafanya mazoezi ili kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kikanda. Naiomba jamii ijitokeze kuja kucheza mchezo huu kwani unafaida nyingi".
Mwansasu alisema mchezo wa gofu unachezwa na rika lolote na kwamba siyo kweli ni wa matajiri.
Mshindi mwingine, Vicky Elias alisema: "Nimefanya mazoezi wiki nzima ninamshukuru Mungu nimeibuka mshindi wa kuiwakilisha nchi. Nawasihi kinadada wekeni bidii katika kufanya mazoezi. Pia wadau wajitokeze kuwekeza na kinamama wawaruhusu watoto wao waje kucheza mchezo huu wa gofu".
Waandaaji wa shindano hilo, ambaye ni Msimamizi wa Masoko, Solomon Frank alisema washindi waliopatikana watashindana na wengine kutoka Rwanda, Kenya, Uganda.
Alisema endapo taifa likiwaandaa vijana kupitia mchezo wa gofu yatapatikana mafanikio mengi ikiwamo uwakilishi wa kimataifa na kulitangaza taifa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED