Yanga yambakiza kikosini Mzize

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 10:31 AM Aug 28 2025
news
Picha Yanga
Picha ikimwonesha mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize (kushoto) akiwa na Rais wa klabu hiyo, Hersi Said, muda mfupi baada ya klabu hiyo kutangaza kumwongezea.

UONGOZI wa klabu ya Yanga hatimaye umevunja 'mzizi wa fitina' baada ya kufanikiwa kumbakisha mshambuliaji wake, Clement Mzize kwa kumwongezea mkataba, imethibitika.

Baada ya tetesi za muda mrefu juu ya usajili wa mshambuliaji huyo akihusishwa kutaka kuondoka katika klabu hiyo na kujiunga na timu ya nje ya nchi, jana Yanga kupitia ukurasa wao wa kijamii walitangaza kumalizana na mchezaji huyo na ataendelea kubakia kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu.

Taarifa inasema nyota huyo amesaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumika klabu hiyo.

Awali, taarifa za usajili za Mzize zilikuwa zikimhusisha nyota huyo kutaka kutimkia katika moja ya klabu Afrika Kaskazini ambayo inatajwa ilikuwa tayari kutoa dau kubwa kwa Yanga na kwa mchezaji mwenyewe.

Tetesi hizo za usajili wa Mzize kwa siku za karibuni ziliibu mvutano huku baadhi ya wadau wakielezea yanga kutaka kumzuia nyota huyo asiondoke.

Mmoja wa viongozi wa Yanga, aliiambia Nipashe jana kuwa wamefanikiwa kumsainisha mkataba mpya Mzize baada ya pande zote kukubaliana na hivyo ataendelea kuitumikia timu hiyo.

"Wana Yanga kwa sasa wasiwe na wasiwasi, Mzize ataendelea kuonekana akiwa na jezi ya timu yetu kwenye Ligi Kuu na Mashindano ya Kimataifa, kila kitu kimeenda vizuri, hakukuwa na shida kwenye mazungumzo mpaka pande zote zimekubaliana," alisema mtoa taarifa.

Taarifa za ndani zaidi zinasema kwa sasa Mzize atakuwa miongoni mwa wachezaji wanaolipwa pesa nyingi zaidi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ambapo inakadiriwa atakuwa akipokea kiasi kinachokaribia Shilingi Milioni 40 kama mshahara wa mwezi.

Pia inaelezwa mshambuliaji huyo wa timu ya taifa 'Taifa Stars' pia amepokea pesa za kusaini mkataba mpya.

Mzize, alikuwa akihusishwa kutaka kutimkia nchii Tunisia kujiunga na Esperance pia akitajwa kutaka kutimkia Ufaransa na Qatar.