Andambwile, Edmund somo la kusaka namba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 03:02 PM Sep 22 2025
Uwanja wa 11 de Novembro jijini Luanda, Angola
Picha: Mtandao
Uwanja wa 11 de Novembro jijini Luanda, Angola

AZIZ Andambwile, kiungo mshambuliaji wa Yanga, ndiye aliyefungua utepe kwa kupachika bao la kwanza nchini Angola, wakati Yanga ikiiadhibu Wiliete de Benguela kwenye ushindi wa mabao 3-0 iliyoupata ugenini.

Hiyo ilikuwa juzi, katika Uwanja wa 11 de Novembro jijini Luanda, ikiwa ni mchezo wa mkondo wa kwanza, mechi ya hatua za awali, Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ni mchezaji alieyejiunga na Yanga msimu uliopita akitokea Fountain Gate. Ikumbukwe kuwa msimu huu ilikuwa chupuchupu aachwe. Ni mchezaji ambaye hakuwa chaguo la kwanza kwa Yanga, kwani wao walikuwa wanamhitaji, Yusuph Kagoma, lakini baada ya dili hilo kufa na akaelekea Simba, wakamchukua Andabwile ili kuziba nafasi hiyo.

Kwa maana hiyo hakusajiliwa kwa mbwembwe na alionekana mchezaji wa kawaida tu. Kwa sasa ni lulu Yanga. Mwenyewe ameshaanza kujitengenezea jina na katika kuthibitisha hilo akafunga bao la kwanza kwenye mchezo wa kimataifa juzi.

Straika Edmund John, amesajiliwa msimu huu akitokea Singida Black Stars. Usajili wake ulikuwa na wa kawaida tu na wala haukuwa na shamrashamra nyingi kwenye mitandao ya kijamii kama baadhi ya waliosajiliwa kwenye klabu hiyo.

Kilichotokea juzi ni kwamba alipachika bao la pili katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga ikitoka na ushindi wa ugenini.

Wachezaji hawa wote wawili wa Kitanzania wanaonesha ni jinsi gani, wanaweza kujipambania wenyewe kupata namba bila kusaidiwa na kelele za baadhi ya wachambuzi, wadau wa soka na kanuni.

Yanga iliwasajili kwa mbwembwe na madaha wachezaji kama Celestin Acua, Moussa Balla Conte, Andy Boyeli na wengineo ambao usajili wao ulifunika kwenye mitandao ya kijamii.

Pamoja na nayo ikilichoonekana ni kwamba wachezaji wa Kitanzania wanaojituma mazoezini wamekuwa wakipata namba na kuwaweka nje wachezaji wa kigeni.

Andabwile na Edmund, wanatukumbusha kuwa maisha inabidi uyapambanie mwenyewe na si kupambaniwa na watu.

Kumekuwa na tabia ya baadhi ya wadau wa soka wakiwemo wanahabari wachambuzi kutaka wachezaji wa nje wawekewe ngumu kwa masharti magumu ili kuwapa nafasi wachezaji wazawa.

Wengine wanataka hadi kanuni ya wachezaji wa kigeni ipunguzwe kutoka 12 hadi 10 na wengine wanataka watano kabisa, lengo ikiwa ni kulinda vipaji vya wazawa.

Mfano mdogo tu ni kwamba tayari msimu huu kuna kanuni inayotaka kipa wa kigeni kuwa mmoja tu kwenye timu.

Binafsi nimekuwa nikipinga hili na kuelekeza kuwa ili wachezaji wetu wawe bora inabidi wapambane wenyewe ili kupata tamba na si kuwawekea urahisi.

Na hili tayari limeshaanza kuonekana kwani, timu zenye wachezaji wengi wa kigeni kama Simba, Yanga na Azam ambako ndiyo wazawa wanabanwa na wageni wengi, ndiko kuna wachezaji wengi wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Kule hakuna wachezaji wa kigeni, badala yake kuwa wabongo watupu na hawabanwi, hakuna wachezaji wa Stars.

Ni ukweli usiopingika kuwa wachezaji wa Kitanzania waliopo Simba, Yanga na Azam, inabidi wapambane kweli kweli  ili wapate namba. Uwapo wa wachezaji wa kigeni unawafanya wafanye bidii mno. Ndiyo maana wachezaji wa timu hizo wa Kitanzania wanapata namba, basi moja kwa moja anakuwa na sifa za kucheza timu ya taifa.

Andambwile na Edmund hawakusubiri kanuni, bali wamepambana wenyewe hadi kocha Romain Folz akaona wanafaa kuanza na kweli wameonyesha hilo mbele ya wachezaji wa kigeni.

Hili ni fundisho kuwa tuwaache wachezaji wa Kitanzania wapambane wenyewe kusaka namba na si kutengeneza kanuni, huruma au uzawa, badala yake uwezo ndiyo utumike.

Hata kama wachezaji wa kigeni wakisajiliwa 20 na wazawa 10, kama hao 10 watajua kilichowapeleka kwenye timu, wanaweza kucheza na kuwaweka benchi wachezaji wa kigeni.

Tuache mchezaji mwenye uwezo mdiyo acheze na si kutengeneza kanuni za kuwatenga wengine kwa ajili ya kuwapa urahisi wachezaji wengine, kisa kwa sababu ni wazawa. Badala ya kukuza, tutaua vipaji vyao kwa sababu atabweteka.

Mwisho.