Bodaboda kupenya si ujanja jalini sheria

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:07 PM Oct 08 2025
Bodaboda usafiri maarufu Dar
Picha: Mtandao
Bodaboda usafiri maarufu Dar

IMEKUWA ni jambo la kawaida kunapokuwa na foleni ndefu ya magari jijini Dar es Salaam vijana wanasikika wakisema hapa mchawi ni bodaboda bwana, na si magari.

Kauli hizo zimekuwa zikisikika pale ambapo magari yanakuwa yamefungana kwa kuingilia barabara zote kutokana na kila dereva kutaka kupita na mwishoni kujikuta amekwama na kukwamisha wengine maana wote hukosa sehemu ya kutokea.

“Hapa bwana mchawi ni bodaboda tu, hebu ngoja tuone…,” anasikika mmoja wao huku akitafuta namna ya kujiondoa kwenye foleni.

 Baada ya hapo unamwona ndani ya pikipiki na mwenye pikipiki pamoja na abiria wake wanachungulia kulia na kushoto kwa kuhama hama na chombo chake cha moto, huku nyuma yake kukiwa na msururu wa bodaboda wenzake wakimfuata kila anakopita. Na huo ndiyo mwanzo wa ajali.

 Maajabu ya hao bodaboda, watu wengi ambao hawakuyajua ni pale wanapojaribu kuchungulia mbele huku akipima kama kichwa chake kinapita kwa kujaribu kwa masikio kulia na kushoto, miguu ikiwa inaburuzwa chini.

 Kisha utashtukia bodaboda kachomoka huku akifuatwa na msafara wa wenzake na kuyaacha magari yakikwama kuendelea na safari kwa kukosa upenyo wa kupita kutokana na ukubwa.

Lakini pia kuna usemi kuwa barabarani hakuna dereva mwenyeji, hapo ndipo ajali na vifo vinapoanzia, hivi karibuni, ilishuhudiwa ajali ya boda katika barabara ya Tabata Segerea jijini Dar es Salaam.

Siku hiyo majira ya jioni, bodaboda huyo akitokea maeneo ya Tabata kuelekea Barabara ya Mandela, alipofika eneo la Aroma, alikuta gari kubwa semi trela likiwa kwenye foleni kwa mwendo wa taratibu.

Kwa kuamiani kwamba angelipita wakati likiwa kwenye tuta, kuwahi alikokuwa akiharakisha huku akiwa amembeba abiria mwanamke, ghafla mbele yake aliliona daladala likija kwa mwendo kasi.

Hatua iliyofuata, bodaboda huyo, ghafla alirudi kwenye upande wake kwa lengo la kujinusuru kugongana uso kwa uso na daladala hilo.

 Kwa imani yake aliiona ile ajali ya daladala kuwa ni kubwa, hivyo njia pekee ilikuwa ni kufaya hivyo, wakati akirudi upande aliokuwa ghafla alilivaa lori lile na kurushwa nje ya barabara na kuangukia kisogo na kupoteza maisha.

 Wakati hayo yakijiri, abiria alitupwa barabarani, akiwa hajitambui kutokana na mshtuko, magari yapatayo matatu yalimpitia mguuni na kuendelea na safari, akiwa ameumizwa kwa kusagwa mguu na kila gurudumu lililompitia.

Watu walioshuhudia tukio la bodaboda huyo kulivaa lori, walipatwa na kiwewe huku wengine wakihamaki kwa vilio hususan wanawake wakisikika kumwita Mungu. 

Siku iliyofuata, bodaboda wengine katika njia ya wanaotembea Barabara ya Nelson Mandela, waligongana uso kwa uso na kusababisha abiria wa mmoja wao, mfanyabiashara wa samaki na maji baridi akitoka maeneo ya Ubungo River Side, kujeruhiwa na wao kuingia mitini.

 Vivyo, hivyo eneo la Darajani Vingunguti yaliko machinjio ya ng’ombe na wanyama wengine, nako kumekuwa kukitokea visa kama hivyo.

 Ajali hizo ni kwa uchache kwani zipo nyingi ambazo zimekuwa zikiripotiwa kutokea kila kona ya nchi, zinazosababisha vifo na ulemavu wa viungo kwa watu kadhaa wa kadhaa.

Jamani vijana wetu tusema sasa inatosha, Tanzania bila ajali za pikipiki inawezekana. Kinachosikitisha vijana wetu mnapotoka nyumbani kwenda kwenye kazi zenu  mmewaacha wazazi, walezi  wanaowategemea baada ya kuwalea hadi mkafikia umri wa kujiajiri na kuajiriwa katika sekta hiyo ya usafirishaji wa bodaboda na kwingineko mnajimaliza, lindeni maisha yenu.

Mkumbuke kwamba nyie ni hazina, mnaacha uchungu mkubwa kwa wazazi, walezi na wategemezi wenu, kuanzia wake na familia. Mnawachia huzuni kwani kila wanapoona vyombo hivyo huwakumbusha machungu yasiyotulizwa.

Pamoja na kuwategemea, mkumbuke pia kuwa ni tegemeo kwa taifa katika sekta nyingi na abiria mnaowabeba pia ni wataalam mnaowabeba na nyie pia mkitegemewa kujenga nchi kumbukeni kuzingatia sheria.