Jipangie na kuishi maisha yako, usiige

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:39 PM Oct 01 2025
Watu
Picha: Mtandao
Watu

KATIKA jamii kuna baadhi ya watu wanapomwona mmoja wao kachukua maamuzi hasa baada ya kukumbukwa na misukosuko ya kimaisha wanatamwona kama kavurugwa au kuchanganyikiwa.

Mifano ninayo mingi ya kuelezea jamii ya watu wa namna hiyo na maamuzi waliyochukua.

Miaka ya 1990, mzee mmoja alipostaafu utumishi wake katika Jeshi la Polisi, aliamua kujiendeleza kwa kusomea sheria baada ya kujiunga na chuo kikuu kimoja nchini.

Watu wengi waliomfahamu wakabaki wakijiuliza kulikoni mzee huyo kujiunga na chuo hicho na kusomea sheria wakati amestaafu akiwa na miaka zaidi ya 55 na anataka nini zaidi katika maisha yake wakati baadhi ya watoto wake ni wasomi wa vyuo vikuu?

Mzee yule akageuka gumzo hadi kwa waliokuwa wafanyakazi wenzake, wafanyabiashara huku watu wengine wakimbeza anataka nini wakati umri wake umekwenda na ataajiriwa wapi na nani?

Kebehi, kubezwa na kuchekwa hakumkatisha tamaa mzee yule, bali aliendelea kupiga kitabu hadi alipohitimu utalamu wake wa sheria aliokuwa akiiupambania akiwa na umri mkubwa.

Umri huo ambao wengi wao hasa watumishi wanaostaafu wanaamua kundelea na maisha yao mengine, kuanzisha miradi ya ujasiriamali, ufugaji na mingine huku wengine wakirudi kijijini wakisema wanarudi nyumbani kufa, wapo wanaorejea mjini kufuata watoto au kuanzisha miradi yao.

Baada ya kuhitimu sheria, alikuwa msaada mkubwa kwa jamii inayomzunguka na watu wengine wengi waliokuwa wakifahamu wakati akiwa ofisa wa upelelezi katika jeshi hilo na mkuu wa waendesha mashataka katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa.

Vilevile alikuwa ni msimamizi wa mafunzo kwa vitendo kwa askari wa jeshi hilo wa upelelezi wa kesi na jinsi ya kuwatambua watuhumiwa wa matukio ya kutisha na wakatumia mwanya huo baada ya kustaafu kwenda kujifunza zaidi.

Mzee huyo, alijenga mazoea ya kutembea kwa mguu kwenda kazini baada ya kuamka alfajiri, hata aliporejea nyumbani kisha kwenda kwa mguu mjini na sehemu nyingine kwa mambo yake mengine.

Kwa wastani kwa siku aliweza kutembea takribani kilomita 20 katika mizunguko yake hiyo kulingana na jiografia ya maeneo aliyokuwa akiishi na familia yake yenye milima.

Pamoja na kufikisha umri mkubwa, alikuwa akionekana na sura ya ujana isiyokuwa na mikunyazi mingi, afya njema, mwenye nguvu, mkakamavu na mcheshi wakati wote

Kwa vyakula, alikuwa akitumia zaidi mbogamboga chukuchuku, matunda hasa mapapai na karanga kiasi.

Ninachotaka kusema ni hiki unaposoma kwa ajili ya mtihani, unaweza kuhisi msongo wa mawazo na kuelemewa na maandalizi yako ya mtihani, lakini unaposoma kuongeza maarifa unashindana na nia yako huna cha kukuumiza.

Aidha, dunia ya leo ni lazima uishi maisha yako usitazame wala kusikiliza wengine wanasemaje, fanya maamuzi wewe si wengine wayafanye kwa ajili yako. 

Kumbuka kuhangaika na kuachana na kuishi mazoea ni sehemu ya kawaida ya maisha ya mwanadamu na mtihani wa maisha unaweza kukupa wakati mgumu japo ni lazima uufanye.

Lakini kuna njia za kudhibiti msongo wa mawazo au changamoto zinazoletwa na mitihani la msingi kudumisha ustawi wako. Kujiwekea tabia nzuri za kudhibiti kufadhaika kutachangia ustawi wako wa kisaikolojia na hatimaye utendaji wako katika masomo.

Inakutia moyo na kukupa changamoto ya kutafuta ukaribu na Mungu kila siku.

Vilevile kufanya mazoezi mara kwa mara kunachochea kemikali zinazoboresha hali ya hewa, huku kukipunguza homoni za msongo wa mawazo na fikra za kujikinai. 

Mazoezi wakati mwingi yanasaidia kuboresha usingizi,hali ambayo ni muhimu kwa kusaidia kuondoa msongo wa mawazo.

Wataalamu wanasema upumuaji wa kina na polepole vinasaidia kupunguza msongo kwa kudhibiti mfumo wa neva wa parasympathetic ambao jukumu lake ni kutuliza mwili.

Inashauriwa kujiwekea wakati mzuri wa kupanga majukumu kwa ajili ya kupunguza hisia za kuvurugika na kuahirisha mambo kwani kunaweza kuongeza msongo.