Kila la heri Simba Day, Wiki ya Mwananchi, amani itawale

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 04:00 PM Sep 08 2025
Mashabiki wa Simba
Picha: Mtandao
Mashabiki wa Simba

NI wiki ambayo mashabiki wa soka, wadau, Watanzania na wengine sehemu mbalimbali Afrika na Dunia, wanakwenda kushuhudia kilele cha matamasha ya klabu mbili na kongwe nchini, Simba na Yanga.

Jumatano kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Simba inakwenda kuhitimisha kilele kwa tamasha walilolipachika jina la Simba Day. 

Unaweza kusema huu umati wote huwa ni kama mtoko, ambapo si wanachama, mashabiki ma wapenzi wa soka tu wanaokwenda, bali hata watu wengine ambao ni wapenda matukio na burudani. 

Huanza kwa burudani ambapo wasanii mbalimbali hupamba tamasha, kabla ya michezo mbalimbali. Baadaye kinachofuata ni kitu ambacho husubiriwa sana na mashabiki. 

Nacho ni kutangazwa mchezaji mmoja mmoja ambaye hutoka kwenye vyumba vya kuvalia na kuja kwa mashabiki uwanjani ili wamwone. 

Shangwe na hoi hoi huwa kwa wachezaji wapya na maarufu, ambao ndiyo hupamba tamasha lenyewe na mwisho inafuata mechi rasmi. 

Jumatano ijayo Simba itacheza dhidi ya timu kongwe Afrika Mashariki na Kati, Gor Mahia kutoka Kenya. Litakuwa ni tamasha la 17 la Simba tangu lilipoanzishwa 2009, lilipoanzishwa mara ya kwanza 2009 chini ya aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo wakati huo, Hassan Dalali. 

La kwanza lilifanyika kwenye Uwanja wa Uhuru (sasa Taifa), Simba ikashinda bao 1-0 lililofungwa na Hilary Eechesa dhidi ya SC Villa ya Uwanda. 

Kwa Tanzania, Simba ndiyo mwasisi wa matamasha haya kwani baada ya hapo, miaka michache baadaye kila klabu ikaanza kufanya matamasha kabla hayo, wakiwemo watani zao wa jadi Yanga. 

Ndiyo maana Ijumaa wakati watani zao wakiadhimisha tamasha la 17, wao watakuwa na tamasha la saba, kwani la kwanza walilifanya 2019. Ilicheza dhidi ya Kariobangi Sharks kutoka Kenya, timu hizo zikatoka sare ya bao 1-1, bao la Yanga likifungwa na Patrick Sibomana, raia wa Rwanda. 

Baada ya hapo nayo iliendelea na utaratibu huo wa kila mwaka, kabla ya kuanza msimu mpya wa mashindano. Kile kile ambacho kinafanywa na watani zao ndiyo hicho hicho kitafanywa nao Ijumaa, lakini yenyewe itamalizia na mchezo dhidi ya Bandari kutoka kule kule, Kenya kama wenzao. 

Ndiyo maana nikasema itakuwa wiki ya pilikapilika sana, mitaani hadi uwanjani. Nizipongeze klabu hizo kwa kuendelea na utamaduni huo ambayo kwa sasa umeenea karibu bara lote la Arika, ambapo siku chache zilizopota hata Yanye wenyewe walialikwa nchini Rwanda kwenye tamasha la Rayon Sports Day. 

Ni matamasha ambayo yanatarajiwa kukusanya watu wengi, hivyo nayatakia si tu kwamba yafanikiwe, lakini yamalizike kwa amani. 

Najua kuwa kumalizika kwa amani bila purukushani, watu kupata tabu ya kuingia, kutoka, kuporwa vitu wakati wa kuondoka, unawafanya mashabiki kuongezeka kwa wingi. 

Tunaliamini Jeshi letu ya Polisi ambalo mara zote lipo imara kulinda watu na mali zao, litafanya kazi kubwa kuhakikisha matamasha hayo makubwa nchini yatamalizika kwa amani ya utulivu kama ilivyo kawaida ili wananchi warejee kwa usalama majumbani mwao kuendelea na shughuli zao za kawaida. 

Kila la keri Simba katika tamasha la Simba Day, Jumatano, na Yanga, kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi, Ijumaa.