Matumizi ya wajibu wa wananchi kidemokrasia

By Beatrice Moses , Nipashe
Published at 03:47 PM Sep 16 2025
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele
Picha: INEC
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele

KAMPENI za Uchaguzi Mkuu nchini zinaendelea kwa kasi, huku wagombea wa nafasi ya udiwani, ubunge na urais wakinadi sera na ahadi za vyama vyao kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara.

Ni wazi kwamba wagombea wanaojitambua wanatimiza wajibu wao, japo binafsi kuna jambo limenishangaza kwa baadhi ya vyama kutofanya jitihada za kuhakikisha sera zao zinapatikana, kwa kifupi ni kwamba wameshindwa kutumia vyema teknolojia ya habari (Teknohama).

Naeleza hivyo kwa kuwa niliamini kwamba kutokana na hali ya baadhi ya vyama jinsi kasi yao ilivyo wangejitahidi kutumia Teknohama ingewasaidia wananchi kupata ilani za vyama vyao ili wapate kuzisoma, ingesaidia kuwapa mwongozo mzuri wa katika kufanya uamuzi wa kupiga kura zao Oktoba 29, mwaka huu.

Pia, naamini kila mpigakura mwenye uelewa anatambua jinsi ya kutumia haki yake ya kidemokrasia kwa busara: Kuchambua, kuuliza na kupima kama yale yanayoahidiwa na wagombea yana uhalisia wa kutekelezeka, sio ndoto za alinacha.

Wachambuzi kadhaa wa masuala ya kisiasa wanabainisha kuwa kuna makundi mawili ya wapiga kura, la kwanza ni lile la wafuasi wa kudumu wa chama fulani, ambalo halihitaji ahadi mpya kuamua, hivyo chama kinakuwa na uhakika wa kupata kura zao wakati wowote.

Kundi la pili ndilo linalobeba hatima ya uchaguzi watu wanaosikiliza hoja, kufuatilia kampeni, na hatimaye kuamua kwa kuzingatia ubora wa sera zinazotolewa ama kujiridhisha na ilani ya chama husika, hivyo hawa wanatajwa kuwa kioo cha demokrasia; kura yao huamuliwa na uwezo wa wagombea kufafanua namna watakavyotekeleza ahadi husika.

Nachukua nafasi hii kuwakumbusha wananchi kuwa hii ni nafasi adhimu kwa wananchi, maana baada ya kura kupigwa, uchaguzi mwingine utasubiri miaka mitano ijayo, hivyo inahitajika umakini wa hali ya juu kujiridhisha ili kuamua nani apewe dhamana ya uongozi.

Jana Septemba 15 dunia imeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Demokrasia. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameonya kuwa demokrasia ipo hatarini kutokana na upotoshaji wa taarifa, mgawanyiko wa kijamii, na kupungua kwa ushiriki wa wananchi.

Amesisitiza kuwa demokrasia inastawi pale ambapo haki za binadamu na uhuru wa msingi vinaheshimiwa, hasa kwa watu walio katika mazingira magumu zaidi.

Ni muhimu pia kutambua kwamba Umoja wa Mataifa, kupitia Mfuko wake wa Demokrasia (UNDEF), umekuwa mstari wa mbele kusaidia taasisi na jamii katika kukuza demokrasia. Ujumbe wa mwaka huu—kutoka Sauti hadi Hatua—unakumbusha kila mmoja wetu kuwa demokrasia sio maneno matupu, bali ni vitendo vinavyohusisha uwakilishi, ushiriki na uwajibikaji.

Kwa Tanzania, ujumbe huu unakuja kwa wakati mwafaka, wananchi wanakumbushwa kuelewa kuwa demokrasia isiyo na ushirikishwaji au inayopuuza makundi fulani ya wananchi sio demokrasia kamili. Wananchi wote vijijini na mijini, vijana na wazee, wanaume na wanawake wanapaswa kushirikishwa na kupata nafasi sawa ya kutoa uamuzi kupitia kura yao.

Jambo jema ni kwamba Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imechukua hatua nzuri ya kuwawezesha wagombea wa nafasi za urais kuwa na usafiri wa uhakika wa kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali kueleza sera zao, kwa hakika wametimiza wajibu wao vizuri.

Kwa wanaoshiriki kampeni na wanaotoa ahadi, wajue kuwa wananchi wanatazama kwa jicho la umakini zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali. Huu sio wakati wa siasa za mihemuko pekee, bali wa siasa zenye mpangilio na uwajibikaji halisi.

Uchaguzi ni kama sehemu ya mtihani kwa demokrasia, hivyo wananchi waache kutoa nafasi ya kutekwa na mhemuko ili washiriki kuchagua viongozi wanaojenga hoja zenye tija na sera zinazogusa maisha ya kila Mtanzania, hapo ndipo demokrasia itakapoendelea kukua na kustawi vyema.